Wednesday, November 28, 2012

Dk. Slaa kinara urais 2015 • Matokeo kura za maoni yawataja Lowassa, Membe na Zitto Kabwe

WAKATI mjadala wa nani anafaa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Serikali ya Jamhuri ya Mungano unashika kasi kila kona ndani na nje ya nchi, jina la Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa limeng’ara, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Pamoja na uwepo wa vyama 18 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, mjadala wa nani anafaa kuwa Rais ajaye, umejikita kwenye vyama vikubwa viwili, kikiwemo Chama tawala cha Mapinduzi (CCM) na Chama Kikuu cha Upinzani cha CHADEMA.
Kwa mujibu wa kura za maoni zilizoendeshwa na mtandao maarufu dunaini wa Jamii Forum kwa kuuliza “Nani ungependa agombee urais mwaka 2015 kwa tiketi ya CHADEMA na CCM”, majina manne yalipambanishwa, mawili kutoka CCM na mawili CHADEMA.
Waliopambanishwa kutoka CCM ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, ambao wamekuwa wakitajwa kuibua makundi yanayosigana kutaka urais mwaka 2015.
Licha ya kuwapo majina mengine yanayotajwa kufaa kuwania urais ndani ya CCM, wapambe wa Lowassa na Membe, wamekuwa katika mvutano mkali na wa wazi na kuibua mpasuko mkubwa ambao ulionekana wazi hata wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.
Baadhi ya majina mengine yanayotajwa kuutaka urais CCM ambayo hayakushindanishwa kwenye kura hizi za maoni ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuri, Steven Wassira, Dk. Emmanuel Nchimbi, Frederick Sumaye na Dk. Asha Rose Migiro ambaye hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa mjumbe wa Sekretarieti ya CCM, akiongoza idara ya mambo ya nje.
Nafasi hiyo inampa sifa Dk. Migiro kuingia kwenye vikao muhimu vya chama vya Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC).
Kwa upande wa CHADEMA, kura za maoni zilizoanza Julai, mwaka huu, ziliwakutanisha Katibu Mkuu na mgombea urais mwaka 2010, Dk. Slaa na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Zitto Kabwe.
Katika siku za hivi karibuni, Zitto amekuwa akijinasibu kutaka kuwania urais mwaka 2015 na kupendekeza sifa ya umri wa kugombea kiti hicho upunguzwe kutoka miaka 40 hadi 35.
Hata hivyo majina mengine yanayotajwa kufaa kuwania urais ndani ya CHADEMA na ambayo hayakushirikishwa kwenye kura hizo za maoni ni pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, ambaye yuko nyuma ya mafanikio yote ya CHADEMA hadi kufikia hatua hii. Katika ordha hiyo, pia yumo Mbunge wa Singida Vijijini, Tundu Lissu.
Matokeo ya kura hizo za maoni, yanaonyesha kuwa jumla ya wapiga kura 1188 walishiriki kuwapigia kura wagombea wa CHADEMA, Dk. Slaa na Zitto, wakati wapiga kura 375 walishiriki kuwapigia Lowassa na Membe, wote kutoka CCM.
Kwa upande wa CHADEMA, matokeo yanaonyesha kuwa Dk. Slaa alipigiwa kura 1,007, sawa na asilimia 84. 76% wakati Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, aliibuka na kura 181, sawa na asilimia 15.
Kwa upande wa CCM, jumla ya washiriki 375 walipiga kura na kati yao, washiriki 164, sawa na asilimia 43.73 walimpigia Lowassa wakati Waziri Membe aliibuka na kura 67, sawa na asilimia 17.87.
Aidha kwa mujibu wa matokeo hayo, wapiga kura 144 walipiga kura ya kutomuunga mkono mgombea yeyote kati ya Membe na Lowassa.
Matokeo ya jumla yanaonyesha kuwa Dk. Slaa aliibuka na ushindi mkubwa wa kura 1,007 kwa kupigiwa kura nyingi zaidi kuliko majina ya washiriki wengine waliopendekezwa kuingia kwenye mnyukano huo.
Mshindi wa pili ni Zitto mwenye kura 181, watatu ni Lowassa mwenye kura 164 na Waziri Membe anashika nafasi ya nne kwa kura 67.
Licha ya kupata kura chache kwenye mchuano huo, jina la Waziri Membe limekuwa likitajwa zaidi tangu alipoibuka mshindi kwenye nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia kundi maalum (Kundi la Kifo), licha ya kupigiwa kampeni chafu na mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), Hussein Bashe, ambaye bila kumung’unya maneno alitamba kumpigia kampeni za kumwangusha asishinde nafasi hiyo.
Hata hivyo matokeo ya kura hizo za maoni sio rasmi kwani kati ya majina yote yaliyoshirikishwa kwenye kura hizo, hakuna hadi sasa aliyekwishatangaza nia ya kuwania urai 2015.

No comments:

Post a Comment