Sunday, November 18, 2012

Rose Muhando, Zunguka kuhamasisha kusaidia watoto yatima Bukoba Des 9

MWIMBAJI maarufu wa muziki wa Injili nchini, Rose Muhando, pamoja na Enock Jonas ‘Zunguka’ wanatarajiwa kutumbuiza katika tamasha maalumu la kuhamasisha kusaidia watoto yatima litakalofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Desemba 9, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kampuni ya Beula Communications Ltd, waandaji wa tamasha hilo, Melkizedeck Mutta, alisema tamasha hilo la aina yake baada ya kufanyika Uwanja wa Kaitaba, baadaye litahamia kwenye ukumbi wa Linas mjini humo.
Alisema lengo la tamasha hilo ni kuhamasisha jamii kuishi kwa amani, kupendana na kusaidia watu wengine hasa wasiojiweza kimaisha ili nao wajione ni sehemu yao, ambapo maandalizi yake yanaendelea vema, huku wadau wengi wakijitokeza kutaka kufanikisha.
“Katika kutambua hilo, kampuni yetu iliamua kufanya utafiti mdogo na kugundua changamoto nyingi katika mkoa wa Kagera, mojawapo ni kuwa na watoto wengi wanaoishi katika mazingira magumu. Baada ya kuliona hili, tulitembelea vituo mbalimbali vya kulelea watoto hao, mojawapo ni kituo cha Tumaini Children’s kinachomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),” alisema.
Aliongeza kuwa kituo hicho kinalea watoto wote bila kujali kabila, jinsia wala dini zao, ambapo kwa sasa kinahudumia zaidi ya watoto 800, kwa kuwapa elimu, chakula, malazi n.k, na kwa muda mrefu kimekuwa kikipata msaada kutoka Sweden, ambao kwa sasa wametangaza kuusitisha kwa maelezo kuwa, jamii ya Watanzania inapaswa kujifunza na kuanza kuhudumia watu wao wenyewe.
“Kutokana na hilo, ndiyo maana tumeonelea tuwe na tamasha la kuhamasisha jamii ili ianze kuona umuhimu wa kusaidia wenzao wanaohitaji msaada,” alisema.
Aliongeza kuwa mbali na wasanii hao, pia kutakuwa na burudani kutoka bendi ya muziki ya wazawa mkoa huo, Kakau Band pamoja na vikundi vingine vya wanakwaya wa makanisa mbalimbali na kikundi cha watoto yatima.
Aidha mkurugenzi huyo aliwaomba wadhamini zaidi na wadau wengine wa maendeleo na watoto, kujitokeza kushiriki ili kusaidia jamii, hasa watoto yatima na wengine wanaoishi katika mazingira magumu.

No comments:

Post a Comment