Sunday, September 2, 2012

CCM NZEGA YATISHIA KUMVUA KIGWANGALA UANACHAMA,ASEMA YUKO TAYARI KUJIUZULU UBUNGE


SAKATA la  makada wa CCM, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangala kutoleana bastola, limechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumnyang’anya bastola Kigwangala huku likianza  kuwahoji wapambe wa mahasimu hao.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, (RPC) Antony Lutta zilieleza kuwa jeshi hilo linaishikilia silaha ya Dk Kigwangala hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

Kauli hiyo ya polisi imekuja siku moja baada ya  uongozi wa chama hicho Wilaya ya Nzega, kutaka suala hilo liondolewe polisi ili walishughulikie kimyakimya ndani ya chama.
Kauli ya Kigwangala
Kwa upande wake Kigwangala alisema kuwa kikao cha Kamati ya Siasa kilivunjika jana kwa sababu hakuwa na imani na wajumbe waliokuwa wakiendesha kikao hicho.

Aliwataja wajumbe wa kikao hicho ambao hana imani nao kuwa ni pamoja na Shija na Katibu wa chama hicho Wilaya ya Nzega, Kajoro Vyohoroka.

Alisema hata kikao cha maadili ambacho kilifanyika baada ya kuvunjika kwa kikao cha Kamati ya Siasa, nacho kina watu ambao hana imani nao.

 ‘’Siwezi kutoa hoja zangu za msingi kwa kamati hii ya maadili, kwani hakuna kilichobadilika kwa sababu wanaokisimamia ni Shija na Vyohoroka na wote wapo upande wa Bashe. Siwezi kukubali kuhojiwa hadi jambo hili litakapopelekwa katika ngazi nyingine ndani ya chama,” alisema Kigwangala.

Alisema siasa za CCM Wilaya ya Nzega ni ‘siasa uchwara’ kwa kile alichoeleza kuwa ni kuwapo kwa makundi yasiyo na msingi wala faida kwa CCM na kusisitiza kuwa kama jambo hilo halitafanyiwa kazi yupo tayari kujiuzulu ili kumwacha Bashe aendeleze siasa uchwara.

“Endapo tatizo hili halitaingiliwa kati na CCM ngazi ya mkoa na taifa, nipo tayari kujiuzulu ubunge na kukabidhi,” alisema Kigwangala.

”Mimi silaha ninayo siku nyingi tu na hata mara moja sijawahi kumtishia mtu maisha, kama unataka kuiona ipo siku nitakuonyesha,” alisema Kigwangala akimwambia mwandishi wa habari hizi.

No comments:

Post a Comment