Sunday, December 2, 2012

Mtanzania anayeishi,kutimiza mila za Kihindi za kuchoma miili ya marehemu

SENTENSI iliyoandikwa katika lango kuu ni ‘Hindu Crematory’, yaani ‘Tanuru la Wahindi la Kuchomea Maiti.’
Ipo katika eneo la Kijitonyama, jijini Dar es Salaam ambalo limetawaliwa na miti mirefu, ikiwamo miembe, mipera na mingine isiyo na matunda. Upande wa kulia, kuna nyumba mbili ndogo nyeupe.
Upande wa kushoto kuna kitu mfano wa kaburi lililosakafiwa vyema pamoja na picha ya mtu anayeonekana kuwa na hadhi kutokana na mavazi yake.
Mbele yake kuna majengo mawili makubwa yaliyoshabihiana kiasi. Yameezekwa juu kwa bati, bali  nguzo nne kubwa zinazoshokilia paa hilo ambalo kwa ndani limesheheni moshi mweusi.
Katikati ya jengo hilo, kuna kitu cha chuma, mfano wa kitanda…na hilo ndilo tanuru la kuchomea miili ya wafu, kama zinavyohubiri mila na tamaduni za Wahindi.
Ndani ya mandhari hii anaishi  Mzee Zuberi Mipiko, mwenye umri wa miaka 79 sasa.
Pamoja na ulinzi, lakini kazi yake kubwa ni kuchoma miili ya wafu.
Mipiko, mwenyeji wa Kisarawe Mkoani Pwani anasema alianza kazi katika tanuru hilo mwaka 1976.
Katika miaka 36 aliyofanya kazi ndani ya tanuru hilo, amekwishachoma maelfu ya miili ya wafu wa mataifa mbalimbali wakiwemo pia Watanzania wenzake.
Mzee Mipiko huwachomaje wafu?

 Kwanza kabisa, anasema baada ya mwili wa marehemu kuingia ndani ya jengo hilo, Wahindi huvunja  nazi tatu katika kaburi lililo karibu kabisa na lango kuu.
Baada ya hapo mwili huletwa katika tanuru lenyewe.  Yeye (Mipiko ) hupanga kuni juu ya tanuru hilo   ambalo limeundwa mithili ya kitanda cha chuma.
“Mimi huanza kupanga kuni kabla hata mwili haujafika ili kuokoa muda kwa sababu huwa napigiwa simu na kuambiwa kuwa leo kuna maiti inakuja,” anasema
Kuni hupangwa kwa ustadi mkubwa. Zile  za ukubwa kiasi hupangwa katika umbile la reli. Magogo makubwa manne hupangwa kushoto, kulia magharibi na mashariki  ya tanuru hilo.
“Kuni zinatakiwa ziwe nyingi kwa sababu kazi ya kuchoma mwili si ndogo,” anasema Mipiko.
 Kabla ya kuuweka mwili katika tanuru, anasema ndugu wa marehemu huuzungusha mara nne, kulizunguka tanuru hilo.
Baada ya hapo, Mwili wa marehemu ukiwa na sanda huwekwa katikati ya kuni hizo, kichwa kikielekezwa magharibi.
Kabla ya uchomaji wenyewe kuanza, mila za Wahindu hasa Baniani, hutaka kuhakikisha iwapo kweli ndugu yao amefariki.  
Ndugu mmoja wa marehemu hutakiwa kuhakiki kwa kuchukua kipande kidogo cha kuni  chembamba kilichoshika moto, kisha humchoma marehemu katika unyayo mara nne, huku akilizunguka tanuru.
“Yaani, anachoma mara moja, kisha anazunguka, na anarudia hivyo hivyo hadi mara nne,” anasema.
Hatua   inayofuata ni kuchukua moto kwa kutumia makoleo maalum, kisha kuuchanganya moto huo na mafuta ya samli.
“Ninachofanya mimi hapo ni kuupaka uso wa marehemu kwa mafuta ya samli, kabla ya zoezi jingine halijaanza,” anasema
Mzee Mipiko anasema husaidiana na ndugu za marehemu kuweka moto na mafuta ya samli katika mwili, baada ya hapo moto huanza kuwaka na kwa kawaida huwa ni mkali zaidi ya gesi.

No comments:

Post a Comment