Wednesday, November 14, 2012

Kaburu arudisha mabasi ya Simba

MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, amerejesha magari mawili ya klabu hiyo yaliyokuwa yanahifadhiwa nyumbani kwake kutokana na wanachama na wadau kudai anatumia mali za klabu hiyo vibaya.
Kwa mujibu wa habari zilizoifikia Tanzania Daima jana, Kaburu ameamua kuchukua uamuzi huo hivi karibuni, baada ya kuona anaandamwa na wapenzi na mashabiki wa timu hiyo.
Chanzo chetu cha uhakika kutoka ndani ya Simba kilisema kuwa, mara baada ya kuandamwa na tuhuma hizo, aliamua kuyarejesha magari hayo aina ya Coaster pamoja na Ice, ambayo yalitolewa na mdhamini mkuu wa klabu hiyo, Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro Premium Lager.
“Ameamua kuyarudisha magari hayo kutoka kwake na sasa yako pale Barabara ya Sam Nujoma, kwa mmoja wa wadau wakubwa wa klabu yetu na hayo yote ni kuepukana na maneno ambayo ameanza kuambiwa, kuwa anatumia vibaya mali ya Simba wakati Kaburu ana mali zake za kutosha,” kilisema chanzo hicho.
Aidha, chanzo hicho kiliongeza kuwa hakipendezwi na kitendo cha matawi ya klabu hiyo kuanza kumsakama Kaburu na kumtaka kuondoka bila ya kuwa na sababu za msingi na kuwa, ni bora wasubiri muda wake umalizike mwakani waweze kumchagua kiongozi ambaye wanamhitaji.
“Wanachama wengi wa matawi ndio wanalivalia njuga suala hili la Kaburu kujiuzulu, kwa kuwa kwa sasa ameyapotezea baadhi ya matawi ambayo yanashindwa kujiendesha yenyewe na kuacha kuwapa fedha kama zamani na ndiyo sababu ya kusema hafai kwa sasa, huu ni unafki, Wanasimba tuache unafki,” kiliongeza chanzo hicho.
Katika hatua nyingine, mtoa habari huyo alisema kamati ya utendaji ya klabu hiyo inatarajiwa kukutana leo kujadili mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuona mwenendo mzima wa timu yao na mambo mengine.
“Kamati inakaa kesho, ingekaa jana lakini Mwenyekiti wetu, Ismail Aden Rage, hakuwepo na ndiyo sababu ya kuahirisha mpaka kesho atakapofika,” kiliongeza chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake kuandikwa gazetini.
chanzo -tanzania daima

No comments:

Post a Comment