Wakati baadhi wakiugulia kwa machungu hayo, kwa
upande mwingine lipo kundi la wale wanaosherehekea neema iliyowajia
mwaka huohuo, baada ya nyota zao kung’ara kisiasa na kujikuta wakikwaa
nafasi za uongozi, pengine ambazo hawakuzitarajia.
Miongoni mwa matukio yaliyowatikisa wanasiasa ni
hatua ya Rais Jakaya Kikwete kupangua Baraza la Mawaziri, kutenguliwa
kwa baadhi ya matokeo ya chaguzi za wabunge na uchaguzi wa ndani wa CCM
ambao uliwaweka kando baadhi ya vigogo wa chama hicho.
Kadhalika, yapo matukio yenye sura ya kipekee
ambayo yanawagusa wanasiasa kama Godbless Lema ambaye alianguka kisiasa
kwa ubunge wake kutenguliwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha mwanzoni
mwa mwaka jana, lakini akaibuka tena shujaa baada ya kurejeshewa nafasi
hiyo na Mahakama ya Rufani, Desemba 2012.
Tukio kubwa ambalo lilitikisa siasa za Tanzania ni
lile la mabadiliko katika Baraza la Mawaziri ambayo yaliwaweka kando
mawaziri sita ambao walikuwa wakiziongoza wizara nyeti zinazosimamia
rasilimali za nchi na huduma za afya na uchukuzi.
Waliong’olewa ni Mustafa Mkulo (Fedha), William
Ngeleja (Nishati na Madini), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omari
Nundu (Uchukuzi), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara) Dk Haji Mponda
(Afya na Ustawi wa Jamii). Pia panga hilo liliwakumba waliokuwa Naibu
Mawaziri, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk Athuman
Mfutakamba (Uchukuzi).
Kuanguka kwa Mkulo, Ngeleja na Maige kulitokana na
taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
iliyozihusisha wizara zao na ufisadi. Dk Mponda na Dk Nkya, waling’olewa
kutokana shinikizo la madaktari ambao walifanya mgomo uliotikisa sekta
ya afya nchini.
Kwa upande wake, Nundu naibu wake, Dk Mfutakamba
waling’olewa kutokana na kashfa ya ujenzi wa gati bandarini ambao
uliwagawa kiasi cha kutofautiana bungeni, wakati Dk Chami naye aliponzwa
na ugomvi na aliyekuwa naibu wake, Lazaro Nyalandu. Hata hivyo Nyalandu
alipona baada ya kuhamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Walioula
Mabadiliko hayo yalikuwa neema kwa wateule wapya
wakiwamo wale ambao hawakuwahi kuwa wanasiasa kama ilivyo kwa Profesa
Sospeter Muhongo ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Profesa Muhongo alipewa naibu wawili; George Simbachawene (Nishati) na Stephen Masele (Madini) ambao walikuwa wabunge.
Wabunge wengine walioula ni Dk William Ngimwa
ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na kupewa naibu wawili ambao nao
hawakuwa katika duru za kisiasa; Saada Mkuya Salum na Janeth Mbene. Ni
wakati huohuo ambao Mwenyekiti wa NCCR -Mageuzi, James Mbatia aliteuliwa
na Rais kuwa mbunge.