Opresheni Linda Tembo. Pambana na Ujangili
Mwaka mzima uliopita, 2012, ulijaa habari za kukamatwa kwa shehena za
meno ya Tembo kutoka Tanzania huko HongKong zikielekea China. Mwezi
Disemba shehena yenye tani 1.3 ya meno ya Tembo iliyofichwa kwenye
magunia ya Alizeti ilikamatwa na Maafisa wa Forodha wa HongKong. Shehena
hii ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni moja na nusu. Wiki
mbili kabla ya hapo takribani tani nne za meno ya Tembo zilikamatwa
huko huko HongKong. Kwa matukio haya mawili, hawa ni sawa na Tembo 900
waliouwawa.
Mwezi
huo huo wa Desemba, 2012 Polisi mkoani Arusha walikamata nyara nyingi
za Serikali katika eneo la Kisongo. Nyara hizi ni pamoja na ngozi za
Simba na wanyama wengine, pembe za ndovu na wanyama wengine na vichwa
vya wanyama. Nyara hizi zilikuwa tayari kwa kuuzwa nje ya Nchi. Mkoani
Katavi walikamatwa majangili kadhaa na kuachiwa huru kwa amri kutoka juu
kwa mujibu wa taarifa za maafisa wa wanyama pori.
Ujangili umeshamiri sana na kwa kasi ya kutisha. Takwimu za Serikali
zinaonyesha kuwa mwaka 2010 jumla ya Tembo 10,000 waliuwawa hapa
Tanzania peke yake. Hii ni sawa na Tembo 37 kila siku. Hali imekuwa
mbaya zaidi mwaka 2012 ambapo jumla ya Tembo 23,000 waliuwawa sawa na
wastani wa Tembo 63 kila siku. Kwa hesabu ya haraka, kutokana na kasi
hii ya ujangili, ifikapo mwaka 2017/2018 Tanzania haitakuwa na Tembo
hata mmoja. Hivi sasa Tanzania ina Tembo kati ya 150,000 na 170,000.
Maafisa wengine wa Wanyama pori wanasema Tembo wanafika 250,000 na nusu
ya Tembo hao wapo pori la Selous kusini mwa Tanzania. Sote tuna wajibu
wa kulinda urithi huu tulioachiwa na MwenyeziMungu.
Kasi ya ujangili imechangiwa na mambo mengi sana lakini kubwa ni
kukua kwa uchumi wa China na nchi nyingine za Kusini Mashariki mwa Asia.
Kwa hiyo takribani nchi zote za Afrika zenye Tembo zinaathirika na
Biashara hii ya Pembe za Ndovu. Tanzania, Kongo-Kinshasa na Msumbiji
zipo kwenye hatari zaidi ya Tembo wake wote kumalizika kutokana na nguvu
kubwa waliyonayo wafanyabiashara haramu wa Pembe za Ndovu. Kenya na
Nigeria inasemekana jumla ya Tembo 25,000 waliuwawa mwaka 2011 peke
yake. Inasemekana kuwa kuongezeka kwa wafanyabiashara wengi kutoka China
na hivyo wafanyakazi kwenye makampuni ya Kichina kuzagaa Afrika
kunachangia kwa kiasi kikubwa sana Ujangili na biashara hii haramu.
Mtandao wa Ujangili ni mpana na wenye nguvu
sana za pesa, kisiasa na kimamlaka. Mtandao huu huanzia chini kabisa
kwenye Mapori na Hifadhi ambapo wauaji ni watu masikini wa vijijini na
wengine hutumia magobole tu. Hawa hulipwa kwa kuua tu. Wakataji nao
huingia hapo na kukata meno na kuandaa usafiri ambao hufanywa wakati
mwingine na magari ya Serikali. Hivi karibuni gari za polisi, muhimbili
na hata magari ya viongozi wa dini yamekamatwa na meno ya Tembo huko
mkoani Iringa. Baada ya kusafirishwa na kufikishwa maeneo ya mijini
hufungwa na kusafirishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam. Katika
mtandao huu kuna watu wa Vijijini, masikini ambao hutumia ujangili kama
sehemu ya kupata kipato. Pia kuna watu wa kati kama maafisa wa Polisi,
maafisa wa wanyama pori, madereva wa magari ya Serikali wenye tamaa tu
kuongeza kipato. Juu kabisa kuna wafanyabiashara wakubwa na inasemekana
pia wanasiasa ambao hulinda biashara hii.
Nina karibia kumaliza kitabu cha kurasa 301 kiitwacho “Killing for Profit: Exposing the illegal Rhino Horn Trade” ambacho kimeandikwa na Mwandishi wa habari Julian Rademeyer wa Afrika Kusini.
Kitabu hiki ni cha uchunguzi ambapo mwandishi amechunguza mtandao mzima
wa biashara haramu ya meno ya Faru. Mwandishi anasema, kule nchi za
Kusini Mashariki mwa Asia kama Vietnam, meno ya Tembo na Meno ya Faru
yana bei kubwa kuliko dhahabu na madawa ya kulevya. Anasema Biashara hii
imejaa tamaa za mali na rushwa ya kiwango cha juu. Mwandishi anaonyesha
kwa ushahidi namna biashara hii ilivyotumika kuendeleza vita Msumbiji
na Angola kwa nguvu ya Serikali ya Makaburu. Hata baada ya ukaburu
kuisha anaonyesha namna ambavyo wanasiasa watawala wanaendeleza biashara
hii na kupata fedha za kampeni.
Katika kitabu hiki Mwandishi anathibitisha kuwa Meno ya Tembo na Meno
ya Faru huko Asia hutumika kama mapambo kwa kutengeneza bangili zenye
bei aghali na kwa matajiri na mapambo mengine kwenye mikufu, herein nk.
Hata hivyo anasema meno haya hutumika kama dawa na hasa dawa za kuongeza
nguvu za kiume kwa wanaume na hivyo kusababisha bei yake kuwa kubwa
sana. Jinsi uchumi wa Mataifa hayo unavyokuwa na kuongeza watu wa tabaka
la kati, ndivyo mahitaji wa Meno ya Tembo na Faru yanaongezeka.
Mwandishi anaonyesha kwamba mwaka 1960 kulikuwa na Faru 100,000 katika
nchi za Zimbabwe na Afrika Kusini. Hivi sasa kuna Faru 2400 tu. Nadhani
ni muhimu kupata pia takwimu za Tanzania kuonyesha hali upande wetu
ipoje. Watafiti waliofanya tafiti kwenye eneo hili watujuze.
Jambo moja lipo wazi hapa Tanzania ni kwamba maeneo ya Hifadhi za
Taifa takwimu za Ujangili ni chache kuliko maeneo ya mapori ya Akiba
kama Selous. Hii inatokana na ukweli kwamba maeneo ya mapori ya Akiba
uwezo wan chi kulinda wanyama ni mdogo sana maana hakuna askari wa
kutosha na waliopo maslahi yao ni madogo sana. Hivyo moja ya pendekezo
la dhati kabisa ni kuimarisha ulinzi kwenye mapori ya Akiba. Pori kama
Selous ambalo ni urithi wa Dunia ni vema liundiwe mamlaka yake (Selous
Games Authority) kama ilivyo Mamlaka ya Ngorongoro. Mapori mengine
yawekwe chini ya wakala wa Serikali na yawezeshwe kutokana na mapato ya
uwindaji wa Kitalii. Lazima kutoa motisha ya kutosha kwa Askari wa
wanyama pori na pia kutoa adhabu kali sana kwa askari atakayejihusisha
na ujangili.
Hata hivyo, wataalamu wa wanyamapori wanasema ‘kuua majangili
hakuleti mafanikio yeyote. Kuna watu wengi sana masikini wapo tayari
kuingia kuua Tembo ili wapate pesa kidogo. Hata ukiua mamia yao,
hawatamalizika. Suluhisho pekee ni kuua soko la biashara hii haramu’.
Soko hili litakufa kwa kuusambaratisha mtandao wa ujangili kwa kuanzia
na wafanyabiashara wakubwa. Hii ndio opresheni. Operesheni linda Tembo.
Sasa ianze. Tafuta namba ya simu ya Mbunge wako au mbunge yeyote
mwandikie “nataka ulinde Tembo wetu #OperesheniLindaTembo kwa kuihoji na
kuiwajibisha Serikali”. Mabadiliko ni Mimi, Ni wewe, Ni sisi. Tumia
simu yako kutaka viongozi wako wawajibike. Ni wajibu wetu kikatiba
kulinda urithi wetu.
CHANZO-ZITO NA DEMOCRASIA
No comments:
Post a Comment