Saturday, January 5, 2013

hospitali ya Aga Khan yapata magari matano

HOSPITALI ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam kupitia mradi wake wa kuungana mkono (JHI) imepokea magari matano ya kubebea wagonjwa kutoka kwa Ndege Medics ambayo yatatumika kusaidia kupunguza vifo vya kinamama na watoto.
Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma ya Afya ya Agakhan Amin Habib(kushoto) akimshukuru Ofisa Mtendaji wa Ndege Medics Dk. Sebastian Ndege, baada ya kupokea magari tano ya huduma ya dharura(ambulance)kutoka kwa Kampuni inayotoa huduma hizo ya Ndege Medics, yenye thamani ya Dola ya Canada 13.5milioni, kulikokuwa sambamba na uzinduzi wa mradi wa kupunguza vifo ya mama na mtoto . Picha na Michael Jamson 
Akipokea msaada huo, Mkurugenzi wa JHI, Sisawo Konteh alisema ili kufikia malengo ya milenia ya mwaka 2015 ya kupunguza vifo vya kinamama na watoto nchini, huduma za haraka zaidi zinahitajika.
“Msaada huu utasaidia kupunguza tatizo hilo kwa kuwa kinamama wataweza kufika hospitali kwa haraka pindi wanapokuwa wagonjwa,” alisema Konteh.
Mradi huo umelenga kuanza katika mikoa mitano ya Tanzania Bara ambayo ni Mbeya, Morogoro, Iringa, Dodoma na Mwanza ambapo kila mkoa utapata gari kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Ndege Insurance, Sebastian Ndege alisema gari hizo zitakuwa zinatoa huduma bure na kuongeza kuwa wana mpango wa kutoa gari lingine kwenda kwenye mikoa iliyobaki.
“Magari haya matano tumeyatoa ili kusaidia kupunguza vifo vingi vinavyotokana na uzazi na ukosefu wa huduma ya haraka pale mama anapotaka kujifungua, hivyo basi nadhani huu ndiyo utakuwa mwarobaini,” alisema Ndege. Aliongeza kuwa thamani ya magari hayo ni Dola13.5 milioni na wao kama wadau wa sekta ya afya watahakikisha wanashirikiana vyema na hospitali hiyo katika mambo mbalimbali kuhakikisha wanafanikisha malengo ya milenia.

No comments:

Post a Comment