Saturday, January 5, 2013

Ving’amuzi Star Times vyalalamikiwa

WAKAZI jijini Dar es Salaam wamelalamikia huduma za ving’amuzi vya Star Times zitolewazo na Kampuni ya Star Media (Tanzania) Ltd kuwa wameshindwa kutoa huduma iliyokusudiwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, wakazi hao walisema kuwa matangazo ya kampuni hiyo yamekuwa na matatizo ya picha na sauti hatua inayosababisha kushindwa kuona picha kwa usahihi.
Mmoja wa wananchi hao, Shabani Juma, alisema kuwa tangu mfumo huo mpya uanze, amekuwa hatumii king’amuzi chake kwa kuwa matangazo yanakwama na kutopata sauti vizuri.
Alisema kuwa ameshangazwa na baadhi ya vituo kupotea bila kuwepo kwa taarifa zozote huku akitolea mfano wa kituo cha Clouds ambacho tangu kuanza kwa mfumo mpya matangazo yake hayaonekani katika king’amuzi hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, William Lan, alisema kuwa matatizo mengi wanayoyapata wananchi ni kutokana na kushindwa kuunganisha antena kama inavyotakiwa.
Alisema kuwa wakati wa kuunganisha antena hizo zinapaswa kuelekezwa kwenye mitambo yao ambayo kwa sasa ipo Kisarawe mkoani Pwani.
“Matatizo mengine yanayosababisha kutoonekana matangazo hayo, ni kwenye maeneo ambayo wateja wetu wanaishi kwa mfano mabondeni, milimani, karibu na majengo pamoja na miti mirefu,” alisema Lan.
Alisema kuwa katika kutatua tatizo hilo wanatarajia kujenga kituo cha kurushia matangazo cha kisasa katika maeneo ya Makongo Kilimani, ambapo kitakamilika ndani ya miezi miwili ijayo kuanzia sasa.
Kwa upande wake Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, David Kisaka alilaumu vikali baadhi ya mawakala wao wanaopandisha bei za ving’amuzi kwa faida zao.

No comments:

Post a Comment