Monday, January 21, 2013

Dk Slaa: Tutaipeleka puta CCM hadi 2015

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa amesema kuwa kuanzia mwaka huu hadi 2015, chama chake kitaipeleka mchakamchaka CCM, kwa kuwa chama chake kimefanikiwa kuwaamsha Watanzania.
Alisema kwamba Watanzania sasa wameamka na kutambua utajiri wa nchi yao na jinsi   rasilimali zinavyotoroshwa nje ya nchi na kuanza kudai kufaidika nazo kwa nguvu. Hivyo Chadema kitaitumia fursa hiyo kuipeleka puta CCM, lengo likiwa kuhakikisha kila Mtanzania anaishi maisha bora.
 
Dk Slaa alisema hayo alipokuwa akizungumza katika kongamano la Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini, ambao ni wafuasi wa chama hicho (CHASO), lililofanyika Dar es Salaam jana.
Alieleza kuwa kinachotokea mikoa ya Lindi na Mtwara, pamoja na maandamano ya hivi karibuni ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ni majibu tosha kwa CCM, kwamba mikutano ya Chadema iliyofanyika mikoa mbalimbali nchini imewaamsha wananchi.
Wanafunzi zaidi ya 500 walihudhuria kongamano hilo kutoka  IFM, Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE) na  Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), pamoja na vyuo mbalimbali vilivyopo Dar es Salaam na mikoani.
Desemba 18 mwaka jana Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alisema kuwa mwaka huu utakuwa ni wa kuunganisha nguvu ya umma kitaifa, baada ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kushindwa kuzifanyia kazi hoja mbalimbali zinazotolewa na chama hicho.
Dk Slaa ambaye alitumia saa 1:06 kuzungumza na wanafunzi hao, alisema kuwa elimu ya uraia waliyoitoa kwa wananchi katika mikutano ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), pamoja na Operesheni Sangara, wamefanikiwa kwa asilimia 99.
“Tumewapa elimu ya uraia wananchi katika mikoa yote nchini na sasa wanajua haki zao,.Hiyo ni kazi na mikutano yetu pamoja na maandamano tuliyoyafanya” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Nawapongeza wanafunzi wa IFM kwa kuandamana, najua wapo watakaosema nachochea maandamano, lakini wanatakiwa kujua kwamba wanafunzi hawa walikuwa na haki, haiwezekani wanabakwa kisha wakae kimya, tena wametoa taarifa polisi na hakuna kilichofanyika.”
Mbali na kutaka Mkuu wa Jeshi la  Polisi nchini, IGP Said Mwema na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kujiuzulu kwa kitendo cha kuamuru  wanafunzi wa IFM kupigwa wakati walikuwa wakililia usalama wao, alisema kwamba kuna tofauti kubwa kati ya vurugu na kudai haki za msingi.
“Inakuwaje polisi wanawapiga mabomu wanafunzi wanaofanya maandamano, lakini wanashindwa kuzuia Twiga wanaotoroshwa nje ya nchi, tuungane, tushirikiane na tupige kelele, ili mali zetu zirudi,” alisema Dk Slaa na kuongeza:

No comments:

Post a Comment