John Mnyika -Nimewasilisha Muswada Binafsi wa Sheria ya kuunda Baraza la Taifa la Vijana
Jana tarehe 4 Januari 2012 niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge taarifa
ya muswada binafsi wa Sheria ya kuunda Baraza la Taifa la Vijana (The
National Youth Council Bill, 2013) kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (1) na
Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).
Nimechukua hatua hiyo
kwa kuwa kwa miaka zaidi ya kumi Serikali imekuwa ikiahidi karibu kila
mwaka bungeni kuwa itawasilisha muswada wa kuunda baraza la vijana la
taifa lakini haijawahi kutekeleza ahadi hiyo; nimeamua kuitekeleza ahadi
hiyo kwa kupeleka bungeni muswada binafsi wa kuunda baraza la vijana la
taifa.
Katika taarifa hiyo ya muswada nimewasilisha madhumuni,
sababu pamoja na nakala ya muswada wenyewe wa sheria ya kuanzisha
Baraza la Vijana la Taifa kwa madhumuni ya kuanzisha chombo cha
kuwaratibu vijana wa Tanzania katika kutekeleza shughuli zao kijamii,
kuuchumi, kiutamaduni na kimichezo, na kuchagiza hali ya utambulisho wa
Kitaifa wa pamoja na uzalendo.
Baraza litawawezesha vijana
kukutana na kushughulikia masuala ya kisera na kisheria yanayogusa
maslahi ya vijana kupitia njia mbalimbali kama zinavyopendekezwa katika
muswada huo katika ngazi na maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika
kitaifa, kiwilaya, kikata na kivijiji/kimitaa.
Muswada pia
utawezesha vijana kuwa na mfuko wa fedha ambazo kwazo vijana wataweza
kutekeleza shughuli hili kufikia malengo ya Baraza ikiwemo ya kuwezesha
utekelezaji wa sera ya taifa ya maendeleo ya vijana.
Muswada
huo umegawanyika katika sehemu nane kama ifuatavyo: Sehemu ya Kwanza ya
muswada huu inatoa utangulizi kwa kutamka jina la sheria na mipaka ya
sheria na tafsiri za maneno yanayotumika kwenye muswada.
Sehemu
ya Pili ya muswada huo inapendekeza kuundwa kwa Baraza la Vijana, kazi
na majukumu yake, na zaidi kuanzisha nafasi ya mwenyekiti wa Baraza.
Sehemu ya Tatu ya muswada huo inapendekeza kuundwa kwa Bunge la Baraza,
Bodi ya Baraza na Bodi ya Washauri wa chama kama sehemu Baraza pamoja
na vyombo vingine.
Sehemu ya Nne ya muswada huo inapendekeza
kuazishwa mfuko wa fedha wa Baraza kwa madhumuni ya kuwezesha
utekelezaji wa kazi za Baraza kama zilivyoainishwa kwenye muswada.
Sehemu ya Tano, ya muswada huo inapendekeza kuundwa kwa sekretarieti
kwa madhumuni ya kuwa watekelezaji wa shughuli za siku kwa siku za
Baraza.
Sehemu ya Sita, ya muswada huo inapendekeza kuanzishwa
kwa Majukwaa ya Vijana katika ngazi ya Halmashauri, na Kamati za Vijana
za Kata, Vijiji na Mitaa kwa madhumuni ya kuzishusha chini shughuli za
vijana kwenye ngazi ya chini kabisa.
Sehemu ya Saba, ya
muswada inapendekeza kusajili asasi na taasisi shiriki za Baraza
zinazoongozwa na vijana na vigezo vitakavyotumika kusajili asasi na
taasisi hizo.
Sehemu ya Nane, ya muswada inapendekeza
kuanzishwa kwa siku na juma la vijana, na zaidi inampa nguvu waziri
kutunga kanuni kwa uendeshaji bora wa shughuli za Baraza.
Itakumbukwa hata kabla kuwa mbunge kwa nyakati mbalimbali nimeungana na
vijana wengine kwa zaidi ya miaka kumi kutaka kuundwe Baraza la Taifa la
Maendeleo ya Vijana kwa lengo la kuwaunganisha vijana bila kujali
tofauti zao zingine katika kushughulikia vipaumbele mbalimbali vya
vijana ikiwemo katika masuala ya elimu, ajira, afya, michezo na maisha
ya vijana kwa ujumla.
Baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge
niliungana na wabunge wengine kuhoji bungeni na serikali iliahidi kwamba
mchakato wa kuundwa kwa baraza hilo ungekamilika katika mwaka wa fedha
2011/2012, hata hivyo mpaka kipindi hicho kinamalizika mwezi Juni 2012
na kuanza kwa mwaka mwingine wa fedha 2012/2013 ahadi hiyo
haijatekelezwa.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
05 Januari 2012
No comments:
Post a Comment