Monday, January 21, 2013

Rais Obama awatukuza Lincoln, Luther King

RAIS Barack Obama wa Marekani ameapishwa rasmi kushika muhula wa pili wa urais, katika sherehe maalumu iliyofanyika kwenye Ikulu ya nchi hiyo jana.
 
Obama ambaye ni Rais wa 44 wa Marekani, aliingia madarakani katika uchaguzi wa kihistoria mwaka 2008 uliomfanya kuwa Rais wa kwanza mwenye asili ya Afrika katika taifa hilo kubwa duniani.
Sherehe za kuapishwa kwake Ikulu jana zilikuwa za faragha na zilihudhuriwa na watu wachache maalumu, leo ataapishwa katika sherehe za jumla zitakazowajumuisha watu wote kwenye Uwanja wa National Mall.
Katika kiapo chake, Obama atatumia Biblia mbili, moja iliyokuwa ikitumiwa na Martin Luther King na nyingine ilikuwa ikitumiwa na aliyekuwa Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln.
Lincoln aliongoza taifa hilo kuanzia Machi 1861 hadi alipouawa Aprili 1865.
Akiwa Ikulu jana, alitumia Biblia iliyowahi kutumiwa na Lincoln, katika sherehe za leo  atatumia Biblia ya Martin Luther King.
Lincoln, ndiye aliyeliongoza taifa hilo kipindi kigumu cha kusimamia umoja na kufuta biashara ya utumwa.
Martin Luther King ambaye alikuwa mchungaji na mwanaharakati wa haki za watu wenye asili ya Afrika nchini Marekani, aliuawa Aprili 4, 1968, muda mfupi baada ya kutoa hotuba yenye nguvu ya I have a Dream (Nimeota ndoto).
Hotuba hiyo ikuwa ikieleza ndoto yake kwamba muda siyo mrefu watu wenye asili ya Afrika watapata nguvu na kupata haki yao kama raia wa Marekani.
Viongozi hao wawili wana historia ya pekee, Lincoln ndiye aliyetumia muda wake mwingi akiwa Ikulu ya Marekani kuhakikisha watu wenye asili ya Afrika ambao walikuwa watumwa wananasuliwa utumwani.
Luther alikuwa mwanaharakati aliyechochea mabadiliko kwa kushinikiza Serikali kuwapa haki zao za msingi.
Obama aliapishwa rasmi jana ikiwa ni siku ya kwanza kati ya siku mbili zilizopangwa, leo ataapishwa mara ya pili katika viwanja maalumu vya Nationa Mall mjini Washington, ambako maelfu ya watu watapata fursa ya kushuhudia.
Hotuba ya kuapishwa kwake  itakayotolewa leo inatarajiwa kuweka historia mpya, pia kuhitimisha matukio ya siku mbili hizi za kuapishwa, ataweka wazi mtazamo wake wa kipindi cha miaka minne ijayo.
Mkusanyiko utakaoshuhudia kuapishwa kwake na kusikiliza hotuba yake moja kwa moja katika uwanja huo unakadiriwa kupungua kutoka ule wa watu 1.8 milioni mwaka 2009 na kufikia kati ya 600,000 na 800,000, huku mamilioni wakishuhudia kupitia televisheni.

No comments:

Post a Comment