JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman amewataka majaji na
mahakimu nchini kulinda heshima na hadhi ya mahakama kwa kudumisha
maadili na uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Jaji Othman alitoa wito huo jana, wakati wa
ufunguzi wa mkutano mkuu wa sita wa Chama cha Majaji Wanawake nchini
(TAWJA) ulioenda sambamba na uzinduzi wa Jarida na Kitabu cha Sheria
zinazotokana na hukumu za kesi mbalimbali (Case Law Manual).
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa mkutano huo, Jaji Othmani alisema maadili ya kazi ndiyo yanaipa heshima Mahakama pamoja na uamuzi wao katika kesi wanazozisikiliza na kuziamua.
“Maadili na uaminifu ndiyo hutupa uhalali kwa wananchi.Majaji na mahakimu wanapaswa kuzingatia uadilifu, katika kusikiliza kesi na kuandika hukumu kwa wakati na za wazi katika hukumu yake.”, alisema Jaji Othman.
Alikipongeza TAWJA akisema kuwa kimekuwa kikizingatia mafundisho hayo ya uadilifu kwa mahakimu, majaji na watumishi wengine wa Mahakama wakiwamo makarani.
Alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili kimeweza kutoa elimu hiyo ya maadili na sheria za jinai na za madai kwa majaji, mahakimu na watumishi wengine zaidi ya 1,000.
Akizungumzia jarida la sheria na mwongozo wa sheria za kesi zilizoamuliwa, Jaji Othman alisema kuwa litakuwa msaada siyo tu kwa majaji na mahakimu bali hata kwa wanafunzi katika vyuo mbalimbali vinavyofundisha elimu ya sheria.
Alikipongeza TAWJA kwa hatua hiyo na kukitaka kuwasaidia majaji na mahakimu kuandika vitabu na majarida mengi zaidi ya kisheria ili kupunguza pengo la uhaba wa vitabu vya kisheria.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Engela Kileo alisema kwa kuzingatia umuhimu wa maadili katika utekelezaji wa majukumu yao, kila mwaka katika mikutano yao wamekuwa na somo la maadili.
Katika hotuba yake alisema kuwa katika mafunzo yao wamekuwa wakiwajumuisha wadau wengine katika utawala wa sheria hususan polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Jaji Kileo alisema kuwa mkutano wao hutanguliwa na somo la uaminifu na kwamba ni sera ya TAWJA kujumuisha mada hiyo kwa maofisa wake kila wanapoendesha mkutano mkuu.
Alisema kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kwa kuzingatia kwamba maofisa wa mahakama wanaozingatia viapo vya ofisi zao ni sehemu muhimu sana katika kuleta imani kwa raia.
Jaji Kileo alisema kuwa ofisa wa mahakama anapaswa kudumisha utawala wa sheria, amani, utulivu na kudumisha demokrasia na maendeleo ya taifa.
“Hali hii inaweza kufikiwa tu kama mhimili wa mahakama utakuwa na maofisa wenye sifa.”, alisema Jaji Kileo.
Alizitaja baadhi ya sifa hizo kuwa ni pamoja na hadhi inayotokana na tabia njema na uaminifu, uvumilivu, uwazi, uimara usawa, busara, ufahamu, huruma, unyenyekevu na uwezo wa kutafsiri na kutumia kanuni za sheria kulingana na hali halisi na kuwasiliana kwa kuzungumza na kuandika.
Akizungumzia uzinduzi wa jarida la kisheria na kitabu cha mwongozo wa uamuzi wa kesi mbalimbali, Jaji Kileo alisema kuwa vyote vinazungumzia masuala mtambuka zikilenga upatikanaji wa haki.
No comments:
Post a Comment