KATIBU Mkuu wa CCM,Abdulrahman Kinana amekerwa na chokochoko za
kidini zilizoanza kujipenyeza hivi karibuhi na kutoa wito kwa madhehebu
ya dini na taasisi zake hapa nchini,kuendelea kuhubiri amani kwa
kuliombea taifa , ili wananchi waendelee kujivunia amani iliyoachwa na
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Kinana alitoa kauli hiyo juzi kwenye maadhimisho
ya siku ya kumbukumbu ya Imam Husein, yanayoadhimishwa na dhehebu la
KhojaShia Ithna Asheri Jamaat Arusha kote duniani na kufanyika kwenye
msikiti wa jumuiya hiyo jijini hapa , ambapo watu mbalimbali wakiwamo
viongozi wa madhehemu pamoja na viongozi wa chama na Serikali
walihudhuria.
Kinana alisema kuwa upo umuhimu mkubwa kwa
viongozi wa dini na taasisi zake kuendelea kuienzi amani kwa kuhubiri
suala la kudumisha amani na kuonya kwamba Serikali haitasita kuchukua
hatua za haraka kwa mtu ama kikundi chochote cha dini kitakachojihusisha
na uvunjivu wa amani.
Alisema pamoja na changamoto zinazojitokeza hivi
sasa kwa baadhi ya dini kukashifu dini zingine ,Serikali ipo macho
kuhakikisha kwamba inadhibiti hali yoyote ya ukiukwaji wa maadili ya
kidini nakusisitiza kwamba dini zote nchini ziendeshe shughuli zake kwa
kuheshimiana.
‘’Usidharau imani ama itikadi ya mtu mwingine
lazima dini ziendeshwe kwa maadili na sio kiholela,kama hupendi
kubaguliwa kwa dini usiwe mwepesi kubagua dini ya mwingine’’alisema
Kinana. Alisisitiza kwa kuyataka madhehebu ya dini kuiga mfano wa
kujenga ushirikiano na mshikamano katika kutangaza neno la Mungu na
kuepuka mifarakano inayoweza kuwagawa watanzania kiimani,na kuwataka
viongozi wa dini kuwa wa kwanza kukemea hali hiyo.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Khoja Shia,
Gulam Hussen alisema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuendelea
kukumbuka mazuri yote aliyokuwa akiyafanya Mtume Muhammad kwa lengo la
kukumbushana na kuyaenzi.
Alisema maadhimisho yao yaliyotambulika kwa jina
la ‘Hussein Day’yanalenga kujenga undugu ,kufahamiana na kupinga ufisadi
unaolinyemelea taifa kwa baadhi ya viongozi wenye tamaa ya
kujilimbikizia mali.
Aliitaka jamii ijifunze kuishi maisha ya kitume
huku ikijali haki na usawa duniani na kuepusha migogoro ya kidini ambayo
haina tija ,aliwataka waislamu wajifunze kuishi kwa upendo.Naye mkuu wa
wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga aliyekuwa amemwakilisha mkuu wa mkoa
wa Arusha, Magesa Mulongo,alisema serikali inatambua mchango wa
madhehebu ya dini katika kuboresha huduma za maendeleo kwa wananchi.
Alizitaka dini zote hapa nchini ziendelee
kudumisha amani na kudai kuwa iwapo amani itaachwa ichezewe ,gharama za
kuirudisha ni kubwa sana hatua ambayo inaweza kusababisha machafuko na
vifo .
Alisema kuwa tayari serikali imepata taarifa kuwa
wapo watu ambao wamekuwa wakijipenyeza kwa ajili ya kuvuruga amani kwa
kutumia mgongo wa dini ,na kusema kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa kila
mwananchi ana uhuru wa kuabudu popote bila kubughudhiwa na kwamba
itakabiliana na wenye nia ya kuleta chokochoko za kidini.
No comments:
Post a Comment