WAKATI Serikali ikiwa imetenga Sh1.5 bilioni kwa ajili ya
ununuzi wa ndege mpya ya Kituo cha Taifa cha Kilimoanga, pamoja na
kusomesha rubani mmoja, imebainika kuwa ndege tatu za kituo hicho,
zilizouzwa kwa kwa Sh500,000 hazijulikani zilipo.
Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati
tofauti, Mkaguzi mkuu wa ajali za ndege nchini, John Nyamwihula na
Mhandisi mkuu wa ndege wa kituo hicho, Gideon Mugusi walisema mara baada
ya ndege hizo kupata ajali, Serikali ililipwa fidia na Shirika la Bima
la Taifa (NIC) .
Nyamwihula ambaye alishiriki katika uchunguzi wa
ndege hizo, alisema tangu NIC iilipe Serikali bima ya ndege hizo, mpaka
sasa hajui ndege zilizouzwa zipo wapi.
Hata hivyo, alisema kati ya mwaka 1986 hadi 1992
kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola fedha hizo zilikuwa ni nyingi
ingawa zilikuwa haziwezi kununua ndege nyingine.
Alisema ndege mbili kati ya hizo ziliharibika
sana, lakini moja Super Cub ilikuwa haijaharibika kwa kiwango kikubwa na
ingetengenezeka lakini wakati ikirejeshwa kituoni hapo kutoka Mpanda,
ndiyo ilikuwa mwanzo wa kuharibika kwake kwani ilisafirishwa kwa gari.
“Ndege hizi zilikuwa zikitumika kudhibiti wadudu
waharibifu wa mazao kama Quelea, Nzige, Mbung’o na wadudu waenezao
Malaria,” alisema Mhandisi Mugusi.
Serikali yatenga Sh1.5 bilioni kufufua kituo
Serikali imetangaza mkakati wa kukifufua tena
kituo cha Kilimoanga kwa ikiwepo kununua ndege moja, kusomesha rubani na
pia kutatua matatizo kadhaa ya kituo hicho.
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Christopha
Chiza alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha kituo hicho, kinafufuliwa
na kufanya kazi ya kupambana na wadudu waharibifu wa mazao.
Alisema katika awamu ya kwanza, Sh1.5 bilioni
zimetengwa ambazo zitatumika katika kununua ndege mpya moja na pia
kugharamia mafunzo ya rubani.
Hata hivyo, wakati Serikali ikiahidi kununua ndege
hiyo moja uchunguzi wa zilipo ndege zilizouzwa bado unaendelea katika
wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi.
No comments:
Post a Comment