Thursday, January 31, 2013

Hifadhi ya Serengeti yatwaa tuzo ya kimataifa

HIFADHI ya Taifa ya Serengeti imeteuliwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Utalii, Hoteli na Huduma za Vyakula kwa mwaka 2013. Uteuzi huu umefanywa na kamati ya uteuzi ya tuzo hizo baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na waandaaji.

Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shulutete alisema Tanapa itapokea tuzo hiyo itakayotolewa kwa Serengeti katika hafla maalumu iliyotarajiwa kufanyika jana mjini Madrid, Hispania.

“Tuzo hizi huandaliwa na taasisi maarufu duniani inayofahamika kama Global Trade Leaders’ Club inayohusisha kampuni zipatazo 7000 duniani,’’ alisema Shelutete.

Alisema tuzo hii ilianzishwa kwa ajili ya kutambua na kuenzi michango inayotolewa na taasisi na kampuni zinazojihusisha na utalii, hoteli pamoja na huduma za vyakula kama njia ya kuthamini mchango na kuhamasisha wale wote wanaofanya kazi katika sekta hii ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi husika.

Shelutete alisema hafla ya utoaji wa tuzo za mwaka huu zilitarajiwa kuhudhuriwa na wadau wa shughuli za utalii kutoka nchi zipatazo 40 duniani na zingeambatana na maonyesho ya kimataifa ya utalii yanayofanyika kila mwaka mjini Madrid, maarufu kama FITUR ambayo Tanzania ni mshiriki.

Hifadhi ya Serengeti ni moja ya hifadhi kongwe nchini ambayo ilianzishwa miaka zaidi ya hamsini iliyopita na ambayo pia ni Eneo la Urithi wa Dunia, kwa sasa hifadhi hiyo ni maarufu kwa wanyama aina ya Nyumbu wahamao kila mwaka katika mzunguko unaohusisha nchi mbili za Tanzania na Kenya. Mzunguko huu wa wanyama wahamao unaaminika kuwa ndiyo pekee uliobakia ulimwenguni unaohusisha wanyama wakubwa wa ardhini.

“Kutolewa kwa tuzo hii ni heshima kwa Tanapa na nchi kwa jumla, ni matokeo ya sera nzuri za uhifadhi zinazosimamiwa na Tanapa katika kuhakikisha kuwa maeneo yaliyotengwa kisheria kama Hifadhi za Taifa yanaendelea kuhifadhiwa vyema kwa ajili ya vizazi vijavyo lakini pia kuhakikisha kuwa viwango vya huduma za utalii katika hifadhi zinakuwa za kiwango cha kimataifa ili kuhudumia wageni watokao sehemu mbalimbali ulimwenguni,” alisema Shelutete.

Tanapa imekuwa katika mchakato wa kuhakikisha inakuza na kutangaza maliasili na hifadhi za Tanzania kwa lengo la kuvutia dunia na watalii katika soko la utalii duniani sambamba na kuingia katika rekodi za kimataifa za masuala ya utalii.

No comments:

Post a Comment