Wednesday, January 16, 2013

Waziri Mgimwa atamba kushusha mfumko wa bei

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa amejigamba kuwa kufikia Juni mwaka huu, mfumko wa bei utakuwa umeshushwa na kuwa tarakimu moja kutokana na mipango maalumu iliyoandaliwa.

Pia, Bodi ya Utendaji ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imeridhia ombi la Serikali ya Tanzania kupewa msamaha wa kukiuka kigezo cha madeni ya nje yenye masharti ya biashara, kwa sababu ukiukaji huo hauwezi kuathiri uhamilivu wa deni la taifa.

Dk Mgimwa alitoa majigambo hayo jana wakati IMF ilipokuwa ikitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari kuhusu kukamilisha kwake mapitio ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania.

Hata hivyo, Dk Mgimwa hakutaka kuelezea kwa undani kuhusu mipango yake hiyo ya kushusha mfumuko wa bei.

Naye Mwakilishi Mkazi wa IMF nchini, Thomas Baunsgaard alisema wameridhia ombi hilo na IMF imekamilisha mapitio ya tano ya utendaji wa uchumi chini ya Mpango wa Ushauri wa Sera za Uchumi na Mapitio ya Mpango wa Msaada wa Tahadhari (SCF).

Alisema bodi imeridhia nyongeza ya Dola 57 milioni za Marekani na kuifanya Tanzania kuweza kunufaika na mkopo wenye masharti nafuu kutoka IMF unaofikia Dola 114 milioni Marekani.

Pia, Baunsgaard alisema bodi hiyo imepitisha mpango wa SCF wa miezi 18 kwa kiwango kinacholingana na Dola 228 za Marekani.
Alisema mkopo huo ni wa dharura iwapo Tanzania itapata matatizo ya uchumi yaliyoyasababishwa na matukio yaliyo nje ya uwezo wake.

Alisema Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IMF, Naoyuki Shinohara katika majadiliano ameipongeza Tanzania akielezea kuwa ina usimamizi mzuri wa sera na maendeleo yaliyofikiwa kuleta utulivu wa uchumi.

“Matarajio kwa muda wa kati ni kwamba mageuzi ya mfumo chini ya mpango huo, yatasaidia kuimarisha uhimilivu wa madeni na kusaidia kupanuka kwa shughuli za uchumi,” alisema na kuongeza:

“Vipaumbele ni pamoja na kufanya mfumo wa kodi ya nyongeza ya thamani VAT kuwa wa kisaa zaidi, kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuboresha usimamizi wa madeni.”
Alisema bajeti ya mwaka 2012/13 imezingatia uwiano mzuri baina ya matumizi ya maendeleo na matumizi katika huduma muhimu za jamii, lengo likiwa ni kudhibiti madeni.

No comments:

Post a Comment