Tuesday, January 15, 2013

Slaa atangaza 2013 mwaka mtakatifu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeufananisha mwaka huu kama mtakatifu, kwa wanachama wake kujiandaa na chaguzi za mwaka 2014 na 2015.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alipokuwa akizindua ofisi za kata na matawi maeneo tofauti ya Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Dk Slaa alisema mwaka huu ni mtakatifu kwa chama hicho, kwa sababu ni pekee uliobaki katika harakati za ukombozi wa Watanzania kabla hawajafikia mwaka 2014.

Aliwataka wanachama na viongozi wa Chadema kufanya kazi zenye kuleta tija kwa wananchi, ikiwamo kufungua ofisi kwa wingi, kuhamasisha wananchi kujiunga kwa wingi na chama hicho.

Alisema lengo ifikapo mwaka wa 2014 ambao ni wa uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka 2015 Uchaguzi Mkuu, kiweze kushika dola.

Dk Slaa ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya kuimarisha chama, kufanya mikutano ya hadahara, alisema licha ya ufunguzi wa ofisi hizo za kata, viongozi na wanachama wahakikishe zinafanya kazi ya kuhudumia wanachama na wananchi siyo kugeuzwa mazalio ya popo au vijiwe. Ili kufanikisha kazi za chama, Dk Slaa aliwataka viongozi hasa madiwani katika siku 365 za mwaka huu, kuhakikisha wanawafikia wananchi kwa njia mbalimbali na kuwaelezea sera za Chadema.

Katika hatua nyingine, Dk Slaa aliwakingia kifua madiwani wa Manispaa ya Moshi kwa kueleza kuwa mara nyingi watu wengi wamejenga tabia ya kulaumu madiwani kila kitu kibaya.

Alisema diwani hashiki fedha, hatoi zabuni na kazi yake ni kuhamasisha maendeleo ya kata husika, ili kuhakikisha miradi iliyopangwa inatekelezwa.

Dk Slaa aliwataka madiwani wa Chadema nchini kuwa mstari wa mbele kusimamia maendeleo ya halmashauri zao.Alisema itakuwa rahisi kwa Chadema kupata ushindi na kumpatia ukombozi wa kweli mwananchi.

No comments:

Post a Comment