Saturday, January 5, 2013

Lema aanza kazi rasmi

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), jana alianza rasmi kazi ofisini kwake huku akiahidi kushirikiana na viongozi wa Serikali wa Wilaya na Mkoa wa Arusha, kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na kutatua kero za wananchi.
Hata hivyo, mbunge huyo alionya kuwa ushirikiano wake na viongozi wa Serikali katika mambo ya msingi yanayohusu maslahi na faida ya umma, hautaathiri harakati zake za kupigania haki na kupinga uonevu, dhuluma na unyanyasaji unaofanywa na viongozi wa Serikali na vyombo vya dola.
“Nitatimiza wajibu wangu kama mbunge pamoja na madiwani wote wa Chadema kwa kushirikiana na viongozi na watendaji wa Serikali, kutatua kero na shida za wananchi. Lakini ushirikiano huu utafanyika bila kupuuza haki za pande zote,” alisema
Alisema kabla ya kuanza kazi rasmi jana, tayari amewasiliana na viongozi wa Serikali wilayani Arusha, akiwamo Mkuu wa wilaya, John Mongela na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas ambapo kwa pamoja wamekubaliana kushirikiana katika mambo ya msingi ya maendeleo na masilahi ya jamii bila shinikizo wala vitisho. Katika hatua nyingine, mbunge huyo alitangaza mambo ya msingi atakayoyasimamia baada ya kurejea ofisini kuwa ni pamoja na kudai haki ya uchaguzi huru wa nafasi ya Umeya wa Jiji la Arusha na upatikanaji wa eneo la biashara kwa wafanyabiashara wadogowadogo (wamachinga) na wanawake wanaouza mboga mboga.
Alisema Jiji la Arusha lina zaidi ya wafanyabiashara ndogo ndogo 15,000 na idadi yao inaongezeka kila siku na kwamba  lazima mamlaka zinazohusika zitafute ufumbuzi wa eneo la kudumu la biashara badala ya kufanya uamuzi wenye harufu za kisiasa kama kuwarundika kwenye eneo dogo la uwanja wa wazi wa mikutano wa Unga Ltd.
Lema alionya kuwa akiwa ni  mbunge, hatakubali kushuhudia kinamama wanaojitafutia riziki kwa kuuza mboga wakichapwa bakora za makalio na mgambo wa Jiji la Arusha.
Pia alitangaza kuwa yuko tayari kushirikiana na wanaCCM watatu waliomshtaki kwa faida, masilahi na maendeleo ya Jimbo la Arusha.
“Ofisi ya mbunge ni ofisi ya wananchi wote bila kujali tofauti zao kiuchumi, kisiasa, kidini wala kabila. Wote, wakiwamo Mkanga (Mussa), Happy (Kivuyo) na Agnes (Mollel) walionishtaki mahakamani waje tujadiliane masuala ya msingi ya maendeleo ya Arusha. sina kinyongo nao,” alisema Lema.
Alisisitiza kuwa sera yake ya kudai haki kwa njia ya maandamano haitakoma iwapo haki haitapatikana kwani ni moja ya njia ya kuonyesha hisia na kufikisha ujumbe kwa wahusika.

No comments:

Post a Comment