Monday, January 28, 2013

Zitto Kabwe Ahoji Asema serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), amemtaka Rais Jakaya Kikwete aende Mtwara ili kusikiliza malalamiko ya wananchi katika sakata la gesi asili badala ya kuendeleza malumbano ya kumtafuta mchawi.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara) na Waziri Kivuli wa Fedha, alisema kuwa kama serikali haitashughulikia suala la Mtwara sasa, yatajitokeza matatizo ya aina hiyo katika mikoa mingine yenye rasilimali zisizonufaisha wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Zitto alisema kuwa, hapa nchi ilipofika ni lazima kwanza kusikiliza kilio cha wananchi wa Mtwara ikiwemo kuelewa madai yao.
“Swali kubwa la watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla ni ‘tunanufaikaje?’ Jibu la swali hili si ahadi za miradi, bali ni vitendo. Hapa ndipo serikali inaposhindwa kushughulikia suala hili, kutoelewa madai ya wananchi na kuyapotosha,” alisema.
Zitto aliongeza kuwa, yafaa viongozi wa kisiasa wenye ushawishi kutoka pande zote, chama tawala na vyama vya upinzani, waende Mtwara kuzungumza na wananchi, lakini wawasikilize kwanza.
Alibainisha kuwa mradi huu wa kutandaza bomba la urefu wa kilometa 542 ni mkubwa sana hapa nchini, na una thamani kubwa zaidi kuliko miradi mingine yote ya miundombinu iliyopata kutokea.
Mradi huu utajengwa kwa mkopo wa dola za Kimarekani 1.2 bilioni kutoka Benki ya Exim ya China.
Alisema kuwa wananchi wa Mtwara kupitia maandamano ya Desemba 27 mwaka jana, wametaka kujua hatma ya maendeleo ya mikoa ya kusini kutokana na mradi huu wa bomba la gesi.
“Serikali imewajibu wananchi hawa kwa kuwaita wahaini, watu hatari na wasioelewa. Imefika mahali inapotosha madai yao kwamba hawataki gesi itoke Mtwara,” alisema.
Katika hilo, Zitto alisema Rais Kikwete ana majibu, hivyo ayatoe sasa kwa wana Mtwara. Kwamba kwa mujibu wa mpango kabambe wa umeme nchini (Power System Master Plan), kulikuwa na mradi wa kufua umeme Mnazi Bay, ambao aliagiza utekelezwe mara moja.
Alisema kuwa serikali ieleze umma kuhusu mradi huo wa kujenga kituo cha kufua umeme 300MW Mnazi Bay, Mtwara na kujenga msongo wa umeme wa 300KV mpaka Singida umeishia wapi?
“Ikumbukwe kuwa Oktoba 12 mwaka jana, Rais Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wa mradi huu kutoka makampuni ya China National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani, ambayo kwa pamoja yalitarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara,” alisema.
Zitto aliongeza kuwa, mradi huo ingehusisha kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida na ungegharimu dola za Kimarekani milioni 684 na kwamba rais aliagiza utekelezwe haraka sana.
“Huu mradi uliishia wapi? Kwa nini serikali ipo kimya kuhusu mradi huu ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa Mtwara?” alihoji.
Zitto alimsifu Rais mstaafu Benjamin Mkapa, akisema ameshatoa kauli kuhusu suala hilo, na kwamba ni wakati muafaka sasa kwa viongozi wengine kumuunga mkono kwa kwenda Mtwara na kukaa na wananchi wa wilaya zote kusikiliza hoja zao na kuona namna ya kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Alisema wakati hatua hiyo inachukuliwa, wananchi waombwe kutulia na kuacha vurugu za aina yoyote ile, na serikali isimamishe mradi mpaka hapo suluhu na wananchi itakapopatikana.
“Serikali iweke wazi mkataba wa ujenzi wa bomba, kwani ni dhahiri gharama za mradi huu ni kubwa mno kulingana na uhalisia wa miradi ya namna hii duniani kote. Katika taarifa zote kwa umma serikali imekuwa ikisema kwamba utagharimu jumla ya dola za Kimarekani 1.2 bilioni,” alisema.
Aliongeza kuwa, katika taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini, iliyotolewa na George Simbachawene kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini juzi, ilisema mradi utagharimu dola za Kimarekani milioni 875. Kwamba usiri katika mkataba huu unaashiria kwamba serikali inaficha kitu.
Zitto alisema kuwa amelazimika kutoa ufafanuzi huo wakati chama chake kikiandaa tamko, kwa lengo la kujibu kile alichokiita uzushi wa Simbachawene alioutoa kwa wahariri, kwamba yeye anachochea wananchi wa Mtwara na kutumika bila uzalendo.
“Vile vile alitoa vielelezo kadhaa kuonyesha kuwa mradi wa kujenga bomba la gesi ni gharama sawa sawa. Akasisitiza kwamba mimi ni mwongo. Katika kipindi chote cha mgogoro wa gesi Mtwara, sijafika Mtwara. Sijafanya mkutano wowote na waandishi zaidi ya kuandika mawazo yangu, kama Mtanzania kuhusu suala hili,” alisema.
Zitto alisema hataki kubishana na naibu waziri huyo ama kiongozi yeyote ya serikali kwa sasa wakati nchi yetu inaungua. Kwamba huu sio wakati wa kutafuta mchawi bali kutafuta majawabu ya changamoto zilizopo mbele yao.
Mtikila anena
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia (DP), Christopher Mtikila, amemtaka Rais Kikwete kutumia hekima katika kumaliza mgogoro wa gesi na maslahi ya Mtwara kinyume chake nchi inaweza kugawanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mtikila alisema kuwa madai ya kwamba umeme wa gesi hiyo ufuliwe kulekule Kusini yanatokana na uchungu wa wananchi wote wa Kusini.
Alisema iwapo moto wa mgogoro huo hautauzimwa kwa hekima, si ajabu ukaimeza mikoa yote ya Kusini ikiwemo Lindi, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Morogoro na hata Rukwa ambapo matokeo yake ni kuzaliwa mataifa mawili mpaka ukiwa reli ya kati.
Mtikila alisema wakazi wa Kusini hawazuii gesi hiyo isitoke bali wanachotaka umeme huo ufuliwe kule kule, lengo likiwa ni kuwaletea mapinduzi ya maendeleo.
“Wananchi wa Mtwara wanafahamu kwamba sumaku ya mandeleo ya uwekezaji wa miradi mikubwa ya kuwaletea maendeleo ni nishati na miundombinu, lakini watawala wa CCM waliwanyang’anya reli ya kusini kwa uharamia wa kung’oa mpaka mataruma na kufutilia mbali hata na tuta lenyewe,” alisema.
Aliongeza kuwa Rais Kikwete analazimika pia kutamka bayana kipaumbele kwa uboreshaji wa bandari kuu ya Mtwara, ikibidi hata kwa kusitisha mradi wa bandari ya Bagamoyo.
Kwamba njia pkee ya kuzima moto huo Kusini na kurejesha amani ni rais huyo kutoa tamko la kukubali kufuliwa umeme huo mkoani Mtwara kwa ajili ya maslahi ya taifa.

No comments:

Post a Comment