Saturday, January 5, 2013

Mwanajeshi wa Lema akamatwa

KIJANA aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, akiwa amevalia sare za Jeshi la Wananchi (JWTZ) katika mkutano wa mbunge huyo uliofanyika Mererani mkoani Manyara na kujitambulisha kuwa anatoka kikosi cha Monduli, amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro juzi baada ya kusakwa kwa siku kadhaa.

Kijana huyo alionekana pichani akiwa amenyoosha vidole viwili kama ishara ya alama inayotumiwa na CHADEMA, na hivyo uongozi wa JWTZ makao makuu kutangaza kumsaka na kumhoji ili kujiridhisha kama ni askari wao, waweze kumchukulia hatua kutokana na kushabikia siasa akiwa amevalia sare za jeshi.
Pia JWTZ walieleza kutilia shaka sare zake wakidai kuwa walishaacha kuzitumia kwa muda mrefu na kwamba kikosi cha Monduli alichojitambulisha kuwa anatoka hakikutajwa jina.
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima, zilieleza kuwa kijana huyo ambaye jina lake bado halijafahamika, alitiwa mbaroni eneo la Boma Ng’ombe na kuhifadhiwa katika kituo cha polisi mjini hapo wilayani Hai.
Hata hivyo, licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa na Msemaji wa JWTZ, Kanali Kampambala Mgawe, kukiri kukamatwa kwa kijana huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alikana akisema hana taarifa za kukamatwa kwake.
Licha ya Kamanda Boaz kukwepa kulielezea tukio hilo, taarifa zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii na kwa baadhi ya wananchi mkoani humo, zilisema kijana huyo alikamatwa na alikuwa akihojiwa na maofisa wa JWTZ kutoka makao makuu.
“Mimi nipo kwenye mkutano na  nimefanya heshima kukupokelea simu yako, hizo taarifa za kukamatwa huyo kijana unazosema zimetokea jana mimi siwezi kujua kwani tokea juzi sina taarifa ya kilichotokea,” alisema Boaz.
Taarifa za awali zilisema kuwa kijana huyo si askari wa JWTZ kama alivyokuwa akijitambulisha kwa watu na kuvalia sare za jeshi hilo, bali alikuwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ambapo hata hivyo alishaacha kazi hiyo.
Akizungumzia kukamatwa kijana huyo, Mbunge wa Arusha Mjini, Lema, alisema kama suala hilo ni kweli basi Watanzania wapo katika hatari kubwa na aibu kwa serikali nzima.
Aliongeza kuwa, ikiwa kijana huyo si askari, ni dhahiri kwa sasa kuna watu wengi wenye kuvaa mavazi ya majeshi tofauti ya Tanzania na kufanya kazi zinazofanywa na askari pasipo kutambuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Kama mtu anaweza kuvaa nguo ya jeshi mbele ya hadhara na akakaa na polisi wetu pasipo kujulikana, unafikiri Watanzania wataendelea kuwa salama?” alihoji Lema.

No comments:

Post a Comment