RAIS Jakaya Kikwete jana alitoa salamu zake za mwaka mpya kwa
kuzungumzia mambo mbalimbali ya kitaifa, huku akibainisha kuwa Bunge la
Katiba, litakaa Novemba mwaka huu kupitisha mapendekezo ya Katiba Mpya.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete alisema Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya maoni
ya mtu mmojammoja nchi nzima na hatua inayofuata ni ya kukusanya maoni
ya makundi maalumu.
“Kazi hiyo ya kukusanya maoni ya makundi maalumu,
itaanza Januari 2013. Natoa wito kwa makundi hayo nayo kushiriki vizuri
kwenye hatua hii muhimu. Baada ya hatua hiyo kukamilika, Tume itaandaa
Rasimu ya Katiba ambayo wanategemea itakuwa tayari Mei, 2013.”
Rais Kikwete alisema Tume itatangaza muundo na
namna ya kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba na baada ya kuwapata
rasimu hiyo ya Katiba itawasilishwa kwenye vikao vya Mabaraza hayo
vitakavyofanyika kati ya Juni na Agosti, 2013.
“Baada ya kukamilika kwa vikao vya Mabaraza ya
Katiba, Tume itakamilisha Rasimu ya Katiba ambayo itachapishwa kwenye
Gazeti la Serikali kama yalivyo matakwa ya sheria. Aidha, itachapishwa
katika magazeti ya kawaida kwa wananchi kusoma.
Novemba, 2013 rasimu hiyo itawasilishwa kwenye
Bunge Maalumu kujadiliwa na kupitishwa. Baada ya Bunge Maalumu kupitisha
itapelekwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kupitia kura ya maoni,”
alisema.
Rais Kikwete alieleza kama kila kitu kitakwenda
kama inavyotarajiwa, Katiba Mpya iliyotokana na maoni na matakwa ya
wananchi itapatikana ifikapo mwaka 2014.
“Mwaka huo Muungano wetu utakuwa unatimiza miaka
50, hivyo hiyo itakuwa zawadi ya tunu kubwa. Tukifanikiwa kupata Katiba
Mpya wakati huo, tutafanya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutumia
Katiba hiyo,” alisema.
Huduma za treni kusambaa Dar
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amewaahidi
wakazi wa Dar es Salaam kuwa Serikali itapanua usafiri wa treni kwa
kuanzisha safari nyingine kutoka katikati ya Jiji kwenda maeneo ya
pembezoni.
Alisema kazi hiyo iliyopangwa kuanza mwaka huu,
inalenga kufikisha huduma za treni maeneo ya Tegeta, Kibaha na Mbagala
Rangi Tatu, huku kukiwa na maboresho stahiki kwa treni zilizokwishaanza
kazi
Rais Kikwete alisema tayari mshauri mwelekezi
ameshateuliwa kufanya upembuzi yakinifu kwenye maeneo hayo... “Tunataka
huduma hiyo iweze kufika Tegeta, Kimara, Luguruni, Kibaha Mbagala Rangi
Tatu na Kongowe. Tuliamua kuanza na reli iliyopo lakini nia yetu ni
kufanya vile hasa inavyotakiwa iwe kwa usafiri wa treni mijini.”
No comments:
Post a Comment