Wanachama wote wa Baraza la
usalama la Umoja wa Mataifa wameunga mkono harakati za jeshi la Ufansa
dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu nchini Mali.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
alisema kuwa anatumai hatua ya jeshi hilo itaweza kurejesha utulivu na
uthabiti nchini humo.Ufaransa iliingilia mzozo huo siku ya Ijumaa baada ya wapiganaji kuanza kusonga mbele Kusini mwa nchi.
Maafisa wa utawala nchini Ufaransa, walisema kuwa wanahofia waasi huenda wakaukaribia mji mkuu Bamako na kusababisha tisho kubwa la usalama katika eneo hilo zima.
Siku ya Jumatatu , baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, lilifanya mkutano mjini New York kufuatia ombi la Ufaransa.
Baada ya mkutano, balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa,Gerard Araud alisema kuwa nchi yake inaungwa mkono na wanachama wote wa baraza la usalama.
Lakini aliongeza kuwa Ufaransa pia ilitaka wanajeshi wa nchi za Afrika Magharibi kupelekwa Mali mara moja.
Hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuunga mkono jeshi la Ufaransa ni ishara ya wasiwasi mkubwa uliopo kuhusu uwezo wa makundi ya kiisilamu yaliyojihami nchini Mali.
Wanadiplomasia wanaonekana kuwa na wasiwasi kuhusu kuwasili kwa wanajeshi nchini Mali kusaidia na harakati za jeshi la Mali dhidi ya waasi.
No comments:
Post a Comment