WAKATI Kikao cha Kumi cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinatarajiwa kuanza kesho, Wabunge watano wamejitokeza kuwasilisha hoja binafsi katika kikao hicho.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Zanzibar Habib Mnyaa
anakusudia kuwasilisha maombi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara kupinga gesi
iliyogundulika mkoani humo kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam.
Naye Waziri Kivuli wa Habari, Vijana,Utamaduni na
Michezo Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alisema atawasilisha hoja binafsi kutaka
kujua fedha zinazotumika kulipia vipindi vya runinga vinavyoelezea
mafanikio ya Serikali.
Mbilinyi ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini
(Chadema) alisema atafanya hivyo ili kujua fedha hizo zinalipwa na nani
kwa malengo gani.
Kwa upande wake, Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM),
Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwasilisha hoja ya kuitaka Serikali
kupeleka bungeni muswada wa sheria, wa kuanzisha Mfuko wa Elimu ya Juu.
Lengo kuu ni kuhakikisha kila mwanafunzi aliyepata nafasi ya kujiunga na
elimu ya juu anakopeshwa kwa asilimia 100.
Naye Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii,
Mchungaji Peter Msigwa anatarajiwa kuwasilisha hoja binafsi kutaka Bunge
liunde Tume ya kuchunguza vitendo vya ujangili vinavyoendelea hapa
nchini.
Kwa upande wake Mbunge wa Msoma Mjini (Chadema),
Vincent Nyerere atawasilisha hoja binafsi kuhusu matukio ya kigaidi na
mauaji holela ya raia wasio na hatia yanayotokea hapa nchini.
Nyerere alisema hivi sasa vitendo vya mauaji
vinaendelea, utasikia polisi kauawa na wananchi au wananchi wamemuua
polisi lakini hakuna hatua zaidi.Analitaka Bunge kutoa maadhimio kuhusu
vitendo hivyo vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao.
No comments:
Post a Comment