MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewahukumu adhabu ya kunyongwa hadi
kufa askari watatu baada ya kupatikana na hatia ya kumuua, Swetu
Fundikira.
Adhabu hiyo ilitolewa jana na Jaji Zainabu Muruke
baada ya kuwatia hatiani wanajeshi hao kwa kosa la kumuua kwa makusudi
Fundikira, kinyume cha kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu.
MT
1900 Sajenti Roda Robert (42) na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid wote wa
JKT Mbweni na MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa Kikosi cha JWTZ
Kunduchi, walimpiga Fundikira, Januari 23 mwaka huu saa 7:30 usiku
wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam na baadaye kufariki dunia usiku
huohuo wa kuamkia Januari 24, mwaka 2010, katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Hukumu hiyo ilifufua upya msiba wa Swetu, baada ya
ndugu zake kuangua vilio, huku chumba cha Mahakama kikigeuka kwa muda
kuwa sehemu ya msiba.
Sambamba na vilio hivyo, ndugu wawili wa
marehemu Swetu walianguka chini na kuzirai kwa muda, kabla ya kupewa
huduma ya kwanza na kurejea katika hali ya kawaida.
Akisoma
hukumu hiyo, Jaji Muruke alisema ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja
kuwa washtakiwa hao ndiyo waliomuua Fundikira, ushahidi uliotolewa na
upande wa Mashtaka (Jamhuri) ulikuwa ni ushahidi wa mazingira, kwamba
Jamhuri imeweza kuthibitisha mashtaka hayo.
Alisema kuwa
anakubaliana na mtiririko wa ushahidi wa upande wa mashtaka kama
ulivyoelezwa na mashahidi wake sita akiwemo daktari aliyeufanyia
uchunguzi mwili wa marehemu pamoja na askari polisi wawili ambao
washtakiwa katika utetezi wao walishindwa kuuvunja.
“Sheria iko
wazi ukiondoka na mtu au ukionekana naye kwa mara ya mwisho na baadaye
mtu huyo akapatikana na madhara, wewe ndiyo unawajibika kutoa maelezo ya
kina kuhusu yaliyompata mtu huyo,” alisema Jaji Muruke na kuongeza;
“Kisheria
ukitoa maelezo ambayo hayajakidhi haja na yana utata ni faida kwa
upande wa mashtaka ambao hutegemea ushahidi wa mazingira. Maelezo ya
kina hayajatolewa na washtakiwa wote.”
Aliendelea, “Ushahidi wa
Jamhuri japokuwa ni wa mazingira, umejengwa thabiti na upande wa utetezi
haukuweza kujenga matundu, ama kuuvunja mnyororo huo, kidole
kinawaelekea wao.”
Jaji Muruke alisisitiza kuwa katika kesi hiyo
licha ya kuwa kuna ushahidi wa kimazingira, upande wa mashtaka umeweza
kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka.
“Hivyo kosa
wanaloshtakiwa nalo limethibitishwa na Mahakama imewaona washtakiwa kuwa
wana hatia ya kumuua Swetu Abdallah Fundikira,” alisema Jaji Muruke,
huku akimuuliza wakili wa Serikali kama washtakiwa wana kumbukumbu
zozote za makosa ya jinai.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali
Mwandamizi aliyejitambulisha kwa jina moja la Kongola alijibu kuwa
hakuna kumbukumbu za makosa ya jinai kwa washtakiwa hao.
Kabla ya
kutoa adhabu hiyo Jaji Muruke alimpa nafasi wakili wa washtakiwa hao,
Karoli Muluge na washtakiwa wenyewe kusema lolote.
Wakili Muluge
aliiomba Mahakama iwape adhabu ambayo ni nafuu kutokana na mazingira ya
kesi hiyo, kwamba umri wa washtakiwa ni mdogo, bado ni vijana ambao ni
nguvukazi ya Taifa na wanategemewa na familia zao.
Mshtakiwa wa
kwanza, Sajenti Robert aliiomba Mahakama impunguzie adhabu akidai kuwa
mama yake ni mjane na anamtegemea na hakuna mtu mwingine wa kumsaidia,
ana watoto wadogo na pia afya yake siyo nzuri.
Hata hivyo, Jaji
Muruke alilazimika kumuamuru mshtakiwa wa pili, Koplo Ngumbe kukaa chini
baada kuanza kujitetea kuwa japo ametiwa hatiani, hakuhusika na mauaji
hayo.
Kwa upande wake, mshtakiwa wa tatu Koplo Rashid aliiomba
mahakama imwonee huruma na impunguzie adhabu akidai kuwa yeye bado ni
mdogo na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza.
Baadaye Jaji Muruke
alisema kuwa ni kweli maombi ya mshtakiwa wa kwanza yanatia huruma na
kwamba mshtakiwa wa tatu hata kumbukumbu zinaonesha kuwa bado ni mdogo
na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza, lakini pia kuna roho iliyopotea.
“Kama
ilivyo ada, ni adhabu moja tu kwa mtu anayepatikana na hatia ya kuua
kwa kukusudia na hakuna mbadala.” alisema Jaji Muruke na kuongeza;
“Hivyo
mahakama hii inatamka kuwa mshtakiwa wa kwanza, mshtakiwa wa pili na
mshtakiwa wa tatu mmepewa adhabu ya kifo, mtanyongwa hadi kufa.”
Baada
ya kutamka adhabu hiyo Jaji Muruke alitoka katika chumba cha mahakama
na ghafla ndugu wa marehemu Fundikira walilipuka kwa vilio ndani ya
Ukumbi wa Mahakama, kama vile walikuwa msibani.
Ndugu wawili wa
marehemu, Mwasiti Fundikira ambaye ni dada wa marehemu na Shelina Hamisi
(mpwa wa marehemu) walianguka chini na kuzirai kwa muda hali
iliyowalazimu watu waliokuwa nao karibu kuwapatia huduma ya kwanza hadi
walipoanza kurejea katika hali zao za kawaida.
Mwanamke mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la Lucy ambaye marehemu alimwacha akiwa na
mimba, alisema kuwa alilia kwa sababu hakuamini kama haki ingetendeka.
Dada wa marehemu, Rehema Fundikira alisema kuwa alikuwa akilia kwa uchungu kutokana na jinsi ndugu yao alivyouawa kinyama.
Wakili Muluge alisema hakuridhika na hukumu hiyo na kwamba atakata rufaa.
Alisema
hakuna shahidi hata mmoja aliyewaona wakimuua na kwamba hata hayo
majeraha yaliyodaiwa kuwa ndiyo chanzo cha kifo cha Fundikira hakuna
aliyeeleza jinsi washtakiwa hao walivyoyasababisha, kama ni kwa kumpiga
au kwa namna nyingine yoyote.
No comments:
Post a Comment