KWA mara nyingine tena, jiji la Mwanza limegeuka kuwa uwanja wa
mapambano baada ya kuibuka mapigano makali baina ya mgambo na
wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Machinga.
Katika mapigano hayo yaliyotokea jana majira ya saa tano asubuhi,
polisi na mgambo hao walilazimika kutumia risasi za moto kujihami na
hivyo kusababisha kifo cha mtu mmoja aliyepigwa risasi na mgambo.
Mbali na kuuawa kwa mtu huyo, pia wengine wawili walijeruhiwa vibaya
kwa risasi katika mapambano hayo yaliyofanyika kwenye makutano ya
barabara ya Pamba, Miti Mirefu na stendi ya zamani ya Tanganyika iliyoko
katikati ya jiji.
Chanzo cha vurugu hizo kinaelezwa kuwa ni mgambo wa jiji waliokuwa
kwenye operesheni ya kuwaondoa Machinga hao kwenye maeneo yasiyoruhusiwa
kisheria kufanya biashara.
Ilielezwa kuwa mgambo hao walifika maeneo hayo ya barabara ya Pamba
kisha kuanza kukamata bidhaa za Machinga na kuondoka nazo bila wahusika
kuwakamata.
Mashuhuda walidai kuwa tukio hilo liliwapandishia hasira Machinga hao
kisha kuanza kuwashambulia kwa mawe askari hao wa jiji ambao baadaye
walilazimika kujihami kwa kufyatua risasi za moto zilizogharimu maisha
ya mmoja wa Machinga hao maarugu kama ‘Chapombe’.
Msako huo ulidaiwa kufanywa kimya kimya na mgambo hao badala ya kutoa
tangazo kwa wahusika kuondoka maeneo hayo kama sheria inavyosema.
“Mimi nimeshuhudia kabisa mgambo wa jiji wakichukua bidhaa za
Machinga, baadaye Machinga nao wakakasirika na kuanza kuwarushia mawe,
ndipo mgambo wakaanza kufyatua risasi wakiwalenga watu,” alisema
shuhuda.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola, alithibitisha
kuuawa kwa risasi mtu mmoja katika mapambano na kumtaja marehemu kuwa
alikuwa mpiga debe.
“Leo zilizuka vurugu kubwa kati ya Machinga na mgambo wa jiji. Vurugu
hizi zilitokea baada ya Machinga kumkimbilia na kumkwida mgambo
shingoni kisha kumtolea sime.
“Baada ya kuona hivyo, mgambo waliokuwa kwenye operesheni walilazimika
kujihami kwa kufyatua risasi hewani, lakini bahati mbaya ilimpata mpiga
debe na kufa papo hapo na wengine wawili walijeruhiwa na wamelazwa
Hospitali ya Bugando,” alisema Matola.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, alieleza kusikitishwa
na vurugu hizo na kusema mgambo hao walikuwa kazini kama walivyopangiwa
katika utaratibu wa kawaida.
Kwa mujibu wa Kabwe, utaratibu na sheria za jiji la Mwanza ni
kuwaondoa Machinga katikati ya jiji na kwamba operesheni ya mgambo ya
kuwaondoa Machinga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria bado
inaendelea.
Hili ni tukio la tatu kwa pande hizo kuzua vurugu tangu kumalizika
Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 na katika matukio yote watu walipigwa na kuuawa
kwa risasi, jambo linalolalamikiwa na wananchi.
No comments:
Post a Comment