MWENYEKITI wa Simba, Ismail Rage amelifunga Tawi la wanachama wa timu
hiyo linaloitwa Mpira Pesa kwa madai ya kukiuka katiba ya klabu hiyo,
pia amevunja kamati zote ndogondogo za timu hiyo.
S
Rage pia
amemfuta uanachama mwenyekiti wa Tawi la Mpira Pesa, Awadhi Masoud
pamoja na Ali Bane kwa madai ya kutoa siri za klabu pamoja na kufanya
ubabaishaji kwa kutumia risiti feki na kushindwa kulipa ada ya uanachama
kwa miaka miwili mfululizo.
Uamuzi huo wa Rage kulifuta
uanachama tawi la Mpira Pesa umekuja siku chache baada ya viongozi wa
tawi hilo kuomba wanachama 698 wa Simba kujitokeza kusaini fomu ili
kuitisha mkutano wa dharura kwa lengo la kujadili matatizo ya klabu hiyo
pamoja na kutokuwa na imani na uongozi wa sasa.
Wanachama hao
waliunda kamati ya kukusanya saini hizo wakiongozwa na Bane
(Mwenyekiti), Masoud (Katibu) na wajumbe Hamis Omar, Chuma Suleiman,
Said Kubenea, Mkoma Hamis, Sophia Lubuva na Omari Mnkonje.
Rage
alisema,"Kuna baadhi ya wanachama siyo waadilifu na wapo kwa ajili ya
kuleta migogoro ndani ya klabu yetu. Nilichoamua na kamati yangu ni
kufuta Tawi la Mpira Pesa pamoja na watendaji wake."
Alisema,"Kama
wanataka kuwa wanachama tena wanapaswa kujiandikisha upya, lengo hasa
ni kumaliza tabia za udanganyifu zinazofanywa na watu wachache."
Pia,
Rage alisema kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo katika mechi za
ligi, kamati yake imeamua kuvunja kamati zote na itaunda upya kabla ya
kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
"Nimeamua kuvunja kamati
zote na nitakaa na kuunda upya. Nataka nichague kikosi upya
kitakachorudisha hadhi ya Simba. Kwa sasa wanachama wanapaswa kuwa
makini na kuisapoti timu yao kwa umoja,"alisema Rage.
Wakati
huohuo, habari kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Simba zinadai kuwa kocha
Milovan Cirkovic ametupiwa virago rasmi na nafasi yake amepewa Twalib
Hilal huku nafasi wa meneja wa timu akipewa Jamhuri Kihwelu 'Julio'.
"Baada
ya mkutano wa juzi viongozi walikubaliana kumtimua Milovan na sasa timu
itakuwa chini ya Hilal na Kihwelu," kilisema chanzo hicho cha habari.
Katika
hatua nyingine, Rage amemwomba radhi nahodha wa Simba, Juma Kaseja
kutokana na kitendo cha kudhalilishwa na mashabiki kwenye mchezo wa Ligi
Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar na kumtaka asahau yaliyopita.
Pia Rage
alikanusha tuhuma za uongozi wa Azam za kudai wao wanahusika kutoa
rushwa kwa wachezaji wa Azam huku akidai wapo tayari kushirikiana nao
katika kutafuta ukweli.
Alisema endapo kiongozi yeyote wa Simba
atabainika kuhusika na jambo hilo atachukuliwa hatua za kisheria ikiwamo
kufutwa uanachama.
No comments:
Post a Comment