WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dk Abdallah Kigoda amesema ni
wakati wa kutochukulia kwa mazoea dhana iliyojengeka kuwa Kilimo ni uti
wa mgongo wa Taifa, bali hata viwanda vina nafasi yake kwa kuwa nchi
mbalimbali zilizoendelea zinategemea viwanda.
Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya ushindani wa Viwanda (Tanzania Industrial Competitive) uliofanyika Dar es Salaam jana.
Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya ushindani wa Viwanda (Tanzania Industrial Competitive) uliofanyika Dar es Salaam jana.
Kigoda alisema ni wakati wa kugeuza fikra kwa kuisaidia sekta ya viwanda na kuwataka wadau wajenge viwanda, na waache kusema kuwa kilimo ndio pekee uti wa mgongo wa taifa.
“Mageuzi ya fikra zetu yanahitajika wakati huu ili tuweze kuleta maendeleo katika nchi yetu, ni lazima tuachane na dhana ya mazoea kwamba uti wa mgongo wa taifa letu ni kilimo pekee, badala yake tuangalie na sekta nyingine kama viwanda kwani nchi nyingi zilizoendelea zimejikita kwenye viwanda pia,” alisema
Kigoda.
Alieleza kuwa ripoti hiyo imejikita zaidi kutatua changamoto mbalimbali inayoikumba sekta hiyo ikiwemo serikali kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji, ubora wa miundo mbinu pamoja na utawala wa kuchukia rushwa na urasimu.
Alisisitiza kuwa kiwango cha biashara katika nchi nyingi za Afrika ni kidogo kulingana na nchi nyingine duniani na kwamba ni 10% kumi tu ya biashara inayofanyika baina ya nchi za Afrika ukilinganisha na nchi ambazo zimeendelea.
Kwa mujibu wa Kigoda katika nchi za Afrika hakuna masoko ya ndani kwa ajili ya kuuza bidhaa, vilevile kuna vikwazo vya biashara na ukosefu wa mtaji fedha jambo ambalo linasababisha kudorora kwa biashara katika masoko ya Afrika.
“Nchi za Afrika zinakabiliwa na ukosefu wa masoko ya ndani, halafu zina vikwazo vingi vya kuendesha biashara na ukosefu wa mtaji kwa ajili ya kuanzisha viwanda jambo ambalo linasababisha kuzorota kwa biashara Afrika,” alisema Kigoda.
Pia alifafanua ni lazima Serikali na sekta binafsi iondokane na dhana ya nadharia na kufanya vitendo kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
“kama tunataka kukuza uchumi wa nchi yetu lazima tuondokane na dhana ya kufanya mambo kwa nadharia, badala yake tujikite kwenye vitendo ili tukuze na kuinua uchumi wa nchi yetu, hili litafanikiwa kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi”, alisema Kigoda.
Mmoja wa waandaji wa ripoti hiyo, Falecia Massak alisema ripoti hiyo imeonesha kuwa katika Tanzania viwanda haviwezi kutengeneza ajira ya kutosha kwani hakuna viwanda vikubwa, na vilevile havijasambaa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Massak alisema viwanda vingi vipo katika jiji la Dar es Salaam na vichache Arusha, jambo ambalo linasababisha kutokuwa na ajira ya kutosha kwani Tanzania ina miji mingi.
No comments:
Post a Comment