KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, ameichambua safu mpya ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) iliyoundwa hivi karibuni mjini Dodoma, akisema wana taswira ya
ufisadi.
Amesema kuwa hali hiyo inatokana na baadhi yao kuhusika kwenye matukio kadhaa ya kifisadi moja kwa moja.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kuhusu mtazamo wake kwa safu hiyo
mpya ya uongozi wa CCM iliyoundwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya
Kikwete, katika mkutano mkuu uliomalizika juzi, Dk. Slaa alisema haoni
jambo jipya.
“Nadhani hakuna jambo jipya, kipya ni kwamba wameteuliwa jana, lakini wote ni wazoefu wachafu,” alisema.
Katika safu hiyo, Kikwete anasaidiwa na makamu wawili, Philip Mangula
wa bara na Dk. Ali Mohamed Shein wa visiwani na pia alimteua kada
mkongwe, Abdullahman Kinana kuwa Katibu Mkuu mpya wa CCM.
Wengine wanaounda Sekretarieti ni Zakhia Meghji, Mwigulu Nchemba,
Asha-rose Migiro, Vuai Ali Vuai, Nape Nnauye na Mohamed Seif Khatib.
Akimchambua mmoja baada ya mwingine, Dk. Slaa alimtuhumu Mangula kuwa
ni mmoja wa watu waliohusika na ufisadi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya
Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania.
“Makamu Mwenyekiti Mangula anahusika na EPA, vimemo vingi vya kutaka
fedha za EPA vimetokea kwake…sioni leo atajisafishaje kuleta tumaini
jipya kwa Watanzania,” alisema.
Kuhusu Meghji, Dk. Slaa alisema huyo ndiye aliyeandika barua na
kudanganya kuwa fedha hizo za EPA zimetoka kwa ajili ya Usalama wa
Taifa.
“Sasa mtu kama huyo aliyedanganya, leo hii ukamweka kwenye fedha maana
yake ni ku-‘recycle material’ ile ile,” alisema Dk. Slaa.
Akimchambua Katibu Mkuu, Kinana, alisema kigogo huyo ana mkono katika
biashara chafu za makampuni ya meli na kwamba hajakanusha mpaka sasa.
Dk. Slaa alisema Kinana ambaye alikuwa meneja kampeni wa mgombea urais
wa CCM mwaka 2010, katika chaguzi hizo CCM imeshutumiwa kwa kuiba kura,
hivyo uteuzi wake ni kukubali kuzika demokrasia nchini.
Alisema timu hiyo imeundwa mahsusi kwa ajili ya kujiandaa kuiba kura mwaka 2015.
Dk. Slaa aliongeza kuwa baada ya uchaguzi, CCM walitumia fedha nyingi
kwa ajili ya kwenda kufanya utafiti wa kukijenga upya chama chao, ambao
uliozaa kauli mbiu ya ‘Kujivua Gamba’, kwamba pamoja na kazi ya
kitaalamu wameshindwa kuvuana magamba.
Alifafanua kuwa hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba walioitwa magamba sasa wamo kwenye safu mpya ya uongozi wa CCM.
Katika kile kinachoonekana kuwa ni kumjibu Rais Kikwete hasa kutokana
na kauli yake kuwa wapinzani wanafanya kazi ya kueneza uongo na kuwataka
makada wa CCM kujibu mapigo, Dk. Slaa alimtaka aache kuwadanganya
Watanzania.
Dk. Slaa alisema kuwa Rais Kikwete huenda hasomi, anadanganywa au anapenda lugha rahisi za kusema wenzake waongo.
“Mawaziri wameutumia Mkutano Mkuu kwa mbwembwe kueleza uongo…katika
ripoti ya Juni 2012, hali ya uchumi wa taifa, iliyoandikwa na Ofisi ya
Rais, Ofisi ya Mipango, na kelele zote zilizopigwa kuhusu maendeleo
yaliyopatikana kwenye barabara.
“Kwenye ripoti hiyo imeandikwa kuwa mwaka 2011 barabara zilizokuwa
katika hali nzuri ni kilomita 5,976 sawa na asilimia 30.4 ya barabara
zote za mikoa,” alisema.
Ukilinganisha na mwaka 2010, barabara zilizokuwa na hali nzuri ni
kilomita 11,012, maana yake ni kuwa nusu ya barabara zilizokuwa nzuri
mwaka 2010 leo mwaka mmoja baadaye ni mbaya.
Aliongeza kuwa wakizitumia takwimu hizo ambazo zimeandikwa na Ofisi ya Rais, bado wanaambiwa ni waongo.
Alisema itakumbukwa kwenye viwanja vya Mwembe Yanga wakati alipotoa
orodha ya mafisadi, Rais Kikwete alimjibu kuwa kelele za mlango
hazimzuii mwenye nyumba kulala lakini leo amekiri ufisadi upo CCM.
Mwanasiasa huyo machachari, alisema kuwa Rais Kikwete amesikika mara
kadhaa akilalamika kuhusu ufisadi ndani ya chama chake na kuhoji kati
yake yeye na Kikwete nani muongo?
“Aidha Rais sio makini; anapenda maneno rahisi…tunamwambia aweke hadharani takwimu asilete propaganda,” alisema.
Slaa alikumbusha pia jinsi ambavyo Rais Kikwete na CCM walivyowaita ni
waongo wakati CHADEMA walipokuja na sera ya matumaini kwa Watanzania
mwaka 2010, wakisema nyumba za tembe na nyasi sasa basi na kueleza
mikakati yao ya kushusha bei ya saruji na vifaa vya ujenzi.
Katika hilo Dk. Slaa alisema kuwa alifurahi juzi kusikia CCM katika
maazimio ya Mkutano Mkuu wao wakisema kuwa watashusha bei ya saruji na
vifaa vya ujenzi.
“Sasa CCM na CHADEMA nani waongo? Mimi nasema hakuna kitu
kinachotushangaza katika uongozi wa sasa, timu ni ile ile ya mafisadi,”
alisema
Aliwataka Watanzania kuwa makini akidai kuwa waliowekwa kwenye safu ya
uongozi CCM ni mafundi wa ufisadi na kutoa wito kuwa wajiandae kulinda
kura.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Samuel Ruhuza, alisema wao kama chama
wanawapongeza CCM lakini kwa jicho la siasa hawaoni kipya na kwamba
viongozi wapya ni wachovu wale wale.
“Hawana jambo jipya kwa sababu CCM imechoka sana haina watu wapya ni
walewale, sasa hivi tulitegemea vijana wapya lakini hilo halijatokea,”
alisema Ruhuza.
No comments:
Post a Comment