Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
CCM kimetangazwa kwamba kitaanza ziara hiyo katika mikoa minne kuanzia kesho huku safu yake mpya ikiongozana na mawaziri.
Nacho Chadema kimetangaza kuwawapeleka
viongozi wake wa juu katika mafunzo ya kuwajengea uwezo kabla ya kuanza
operesheni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) itakayofanyika nchi
nzima kuanzia Februari mwakani.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na
Mawaziri wa Wizara mbalimbali kesho wanatarajia kuanza kukagua
utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ya mwaka mwaka 2010.
Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape
Nnauye alisema jana kuwa, ziara hiyo iinatarajia kuanza katika mikoa ya
Mtwara, Geita, Rukwa na Arusha.
Alifafanua kuwa katika ziara hiyo, Kinana atapata maelezo ya kina juu ya utekelezaji wa Ilani hiyo.
“Ni muhimu Mawaziri kuelezea juu ya
utekelezaji wa Ilani kwa kuwa Chama hiki ndicho chenye mkataba na wapiga
kura, hivyo lazima kiwabane mawaziri wa serikali inayotokana na Chama
hiki ili kuitekeleza,” alisema Nape alipozungumza na waandishi wa
habari.
Alisema ziara hiyo ni miongoni mwa maazimio ya Mkutano Mkuu wa CCM uliomalzika hivi karibuni mkoani Dodoma.
Hii ni mara ya pili CCM kufanya ziara
mikoani ikiwa na Mawaziri. Mapema mwaka huu, viongozi hao walizunguka
maeneo mbalimbali ya nchi kuelezea utekelezaji wa Ilani kwa wananchi.
Kwa upande wake, Chadema kimeanzisha
mpango wa kuwapa mafunzo viongozi wa kitaifa na watendaji wa Makao Makuu
pamoja na wenyeviti na makatibu wa mikoa ili kuwajengea uwezo kwa ajili
ya maandalizi ya operesheni ya M4C itakayoanza kutikisa nchi Februari
2013.
Katika orodha hiyo, wamo wenyeviti na
makatibu wa mikoa wapatao 64 na baada ya mafunzo hayo, chama hicho kwa
siku kitakuwa kinafanya mikutano ya hadhara 239 katika vitongoji,
vijiji, kata na wilaya kwenye mikoa yote nchini ili kuimarisha mchakato
wa mabadiliko.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa
Chadema, Benson Kigaila, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini
Dar es Salaam, alisema mafunzo hayo ambayo yataanza Novemba 22 hadi 23
mwaka huu, pia yatahusisha viongozi wa kitaifa na watendaji wa Makao
Makuu.
Kigaila alisema siku mbili za mafunzo
hayo ambayo yatafanyika Wilaya ya Karagwe Mkoa wa Kagera, zitakuwa ni
kwa ajili ya mafunzo ya darasani na baada ya hapo wenyeviti na makatubu
hao watasambazwa katika vitongoji na vijiji vya wilaya hiyo kufanya
mikutano ya hadhara.
“Mafunzo haya ya darasani na vitendo ni
sehemu ya utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya ujenzi na uimarishaji wa
Chama, hususani kupitia Vuguvugu la Mabadiliko ambayo moja ya malengo
yake ni kuwajengea uwezo viongozi kwa kuzungumza na wananchi katika
mikutano ya hadhara,” alisema Kigaila.
Kigaila alisema baada ya mafunzo hayo,
wenyeviti na makatibu hao watarudi katika maeneo yao kwenda kutoa
mafunzo kwa wilaya na majimbo yote ya mikoa ambao nao pia watashusha
elimu hiyo kwenye kata, vijiji na vitongoji.
Alisema baada ya mafunzo hayo kufikia
katika ngazi ya chini ya uongozi wa chama, operesheni M4C itakuwa
inafanyika kwa ngazi zote nchi nzima kwa kufanya mikutano ya hadhara
239.
“Tunataka kuwasha moto nchi nzima ili
tuone kama CCM watakuwa na ubavu wa kujibu mapigo kama ambavyo
wameelezwa kuwa wawe wanajibu mapigo ya wapinzani,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment