MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), amemfutia kesi mmoja wa washtakiwa
waliojumuishwa katika kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake.
Pia katika
kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hakimu
ameuamuru upande wa mashtaka uache utaratibu wa kumwingiza mahakamani
mshtakiwa wa kwanza, Sheikh Ponda akiwa amefungwa pingu.
Aliyefutiwa mashtaka jana ni mshitakiwa wa 35 katika kesi hiyo, Rashid Omar.
Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka ndiye aliyetoa taarifa kuhusu
uamuzi huo wa DPP wakati wa usikilizwaji wa maelezo ya awali wa kesi
hiyo jana.
Kweka aliieleza mahakama kuwa, DPP kupitia kifungu cha
91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hana nia ya
kuendelea na mashtaka dhidi ya Omar.
Kutokana na uamuzi huo wa DPP, Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo aliamuru mshtakiwa huyo aachiwe huru.
Hata
hivyo, wakati mshtakiwa huyo akiachiwa huru, Kiongozi wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mukadamu Abdallah Swalehe aliunganishwa
katika kesi hiyo.
Sheikh Swalehe alipandishwa kizimbani hapo kwa
mara ya kwanza Novemba 2, 2012 na kusomewa mashtaka manne likiwemo la
wizi wa mali ya Sh59.6 milioni, mashtaka ambayo yanahusiana na mashtaka
ya Sheikh Ponda na wenzake waliopandishwa kizimbani kabla yake.
Hatua
ya Sheikh Swalehe kuunganishwa na wenzake, ilisababisha upande wa
Jamhuri ubadilishe hati ya mashtaka na kisha kusomwa upya.
Kwa
mujibu wa hati hiyo mpya, washtakiwa wote 50 wanakabiliwa na mashtaka
manne kwa pamoja, lakini Sheikh Ponda na Sheikh Swalehe walisomewa
shtaka lingine zaidi na kufanya wawe na mashtaka matano.
Mashtaka
yanayowakabili washtakiwa wote ni wizi, kula njama, kuingia kwa nguvu
kwenye eneo lisilo mali yao kwa nia ya kutenda kosa na kujimilikisha
ardhi kwa nguvu na kusababisha uvunjifu wa amani.
Shtaka la tano
ambalo linawakabili Sheikh Ponda ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika
kesi hiyo na Sheikh Swalehe ambaye ni mshtakiwa watano ni la uchochezi.
Katika
hatua nyingine, Hakimu Nongwa aliamuru Ponda asiingizwe mahakamani
akiwa amefungwa pingu na badala yake aliitaka Jamhuri itafute utaratibu
mwingine wa ulinzi, badala ya kutumia pingu hadi mahakamani.
Hatua
ya Hakimu inatokana na maombi ya Wakili wa utetezi, Juma Nassoro
aliyelalamikia utaratibu wa Ponda kuingizwa kwenye chumba cha mahakama
akiwa amefungwa pingu mikononi.
Maelezo ya awali
Baada ya kusomewa mashtaka hayo upya, washtakiwa hao walisomewa maelezo ya awali ya mashtaka yanayowakabili.
Kweka
alidai kuwa, Oktoba 12, 2012, washtakiwa hao walivamia kiwanja cha
taasisi iitwayo Agritanza Ltd kilichopo Chang’ombe,Temeke jijini Dar es
Salaam na waharibu msingi wa nyumba uliokuwa umeshajengwa.
Wakili
Kweka alidai kuwa, washtakiwa walivamia kiwanja hicho kwa nguvu
wakiongozwa na mshtakiwa wa kwanza (Ponda) na mshtakiwa wa tano
(Swalehe) na kwamba, walikuwa wakikaa hapo hadi walipokamatwa Oktoba 16,
mwaka huu.
Alieleza kuwa, Agritanza Ltd waliuziwa kiwanja hicho
na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakatwa) ambayo ni taasisi
iliyoundwa na kusajiliwa kisheria kutoa miongozo kwa Waislamu.
Alidai
kuwa, chini ya wadhamini wake, Bakwata inamiliki mali mbalimbali
zikiwemo majengo na viwanja, kikiwemo cha Chang’ombe Markazi,
wilayaniTemeke, jijini Dar es Salaam.
Wakili Kweka aliendelea
kudai kuwa, Juni 18, 2011 Bakwata kupitia bodi ya wadhamini wake
iliingia makubaliano na Kampuni ya Agritanza Ltd kuuziana au
kubadilishana kiwanja hicho.
Alidai kuwa, katika kuuziana kiwanja
hicho, Bakwata walikubaliana na Agritanza walipe fedha pamoja na kuipa
Bakwata kiwanja kingine kilichopo mkoani Pwani na kwamba, tangu siku
hiyo umiliki wa kiwanja hicho ukahamishiwa kwa Agritanza.
Wakili wa utetezi
Hata
hivyo washtakiwa hao, kupitia kwa wakili wao Nassoro waliyakubali
majina yao na kuwepo kwa chombo kinachoitwa Bakwata, lakini wakakana
kuwa chombo hicho ni kwa ajili ya Waislamu wote, wakidai kuwa ni kwa
ajili ya baadhi ya Waislamu tu.
Kadhalika aliomba washtakiwa
wapewe maelezo ya mlalamikaji, orodha ya mashahidi pamoja na vielelezo
vitakavyotumiwa na upande wa mashtaka.
Akijibu hoja hizo, Kweka
alidai kuwa kutoa orodha ya mashahidi wake pamoja na vielelezo si
matakwa ya kisheria, hivyo Jamhuri haiwezi kulazimishwa.
Hakimu
Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29, 2012 itakapoanza
kusikilizwa mahakamani hapo. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo wako
nje kwa dhamana isipokuwa Ponda na Swahele tu ambao dhamana yao
imezuiliwa na DPP.
No comments:
Post a Comment