Sunday, November 18, 2012

Mwili wa Makwetta kuagwa leo

MWILI wa Waziri wa zamani wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Jackson Makwetta aliyefariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), unatarajiwa kuagwa leo kuanzia saa 10:00 jioni nyumbani kwake, Boko kwa Wagogo nje kidogo ya Dar es Salaam.
 
Taarifa iliyotolewa na familia yake kwa vyombo vya ilieleza jana kuwa maandalizi yote kwa ajili ya shughuli hiyo yanaenda vizuri na mwili huo utaandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Taarifa hiyo ilieleza kwamba mara baada ya kuaga mwili utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na utasafirishwa mapema alfajiri kesho Jumanne kwa ndege kwenda Njombe mkoani Iringa.
"Ndugu wachache watasafiri na mwili wa marehemu na wengine watafuata kwa magari na maziko yanatarajiwa kufanyika keshokutwa Jumatano saa sita mchana kijijini kwake Agafilo," ilieleza taarifa hiyo.
Makwetta alifariki juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alipelekwa akitokea Hospitali ya Jeshi Lugalo ikiwa ni safari ya kutokea katika Hospitali ya Ikonda wialayani Makete ambako alilazwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo.
Makwetta ambaye alifariki muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoka kumjulia hali, alizaliwa Juni 1943 na katika uhai wake alipata kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kati ya mwaka 1976-1980.
Pia amepata kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na kuwa Waziri wa Nishati na Madini (1982-1983), Waziri Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (1989-1990), Waziri, Kilimo na Chakula (1983-1987) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (1987-1990).
Makwetta pia aliwahi kushika wadhifa wa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi (1989-1990), akarudishwa tena wizara ya Kilimo na Chakula (1991-1992) na pia amewahi kushika nafasi ya Waziri wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu (1995-1998).
Makwetta ambaye alikuwa mbunge wa Jimbo Njombe tangu 1975 hadi 2005 alipoenguliwa katika kura za maoni, ameshika nyadhifa tofauti katika awamu tatu za uongozi wa nchi kuanzia awamu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere hadi awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa.

No comments:

Post a Comment