Mabilioni ya Uswisi – Tusigeuzwe Mazezeta
Jumanne tarehe 20 Novemba 2012, baadhi ya vyombo vya habari vimebeba
habari zinazohusu matamshi ya Waziri wa Utawala Bora ndugu George
Mkuchika kuhusu sakata ya mabilioni ya Uswisi. Waziri amesema kwamba
Serikali ya Uswisi inataka majina ya Watanzania walioficha fedha huko
ndio waweze kusaidia uchunguzi. Habari kama Hiyo, yenye maudhui na
malengo hayo hayo iliandikwa na Gazeti la The Guardian on Sunday la
tarehe 18 Novemba 2012.
Nimeona ni vema nitoe kauli yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo ni
kuweka rekodi sawa juu ya Azimio la Bunge na kwamba Serikali inapaswa
kutekeleza Azimio na sio kutoa kauli tata za kukata tamaa.
Moja, Suala hili japo sio jipya lakini limeandikwa kama ni jambo
jipya. Suala la Serikali ya Uswisi kutaka majina lilisemwa na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akichangia hoja binafsi
niliyowasilisha Bungeni na pia wakati akileta maombi yake ya kuiondoa
hoja ambayo yalikataliwa na Bunge. Kama sio sababu mpya ni kwanini
imeibuka upya na kwa kasi? Ni wazi Serikali inajihami kwa kuona kuwa
itashindwa kutekeleza azimio la Bunge. Watanzania wasikubali propaganda
hii ya Serikali. Bunge limeagiza Serikali kufanya uchunguzi kwa kutumia
njia za kiserikali au wachunguzi binafsi wa kimataifa. Kwa nini Serikali
inaanza kubwabwaja ilhali wala haijaanza kazi hiyo? Serikali inajaribu
kuficha nini? Kwa nini baada ya wiki iliyopita Benki Kuu kufanya
uchunguzi kwenye Mabenki ya Biashara jijini Dar es Salaam na namna fedha
zimekuwa zikipelekwa nje (international transfers), leo Serikali
inakuja na kauli za kukakata tamaa? Kunani?
Pili, Watanzania wajue kwamba Taifa la Swiss limejengwa na linajengwa
kwa fedha hizi za wizi ambazo watu mbalimbali duniani wanaiba au
kukwepa kodi kwenye nchi zao na kuzificha huko. Serikali ya Swiss hata
siku moja haiwezi kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika
suala kama hili. Ndio maana Azimio la Bunge linataka wachunguzi binafsi
ambao hawatahitaji ushirikiano wa Serikali ya Swiss. Nawakumbusha kwamba
mwaka 1997 mara baada ya Joseph Desire Mobutu kuangushwa na Rais Joseph
Kabila kule Kongo – Kinshasa, Serikali ya Swiss iliitaka Serikali ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuonyesha ushahidi kuwa hela hizo za
Mobutu zilikuwa zimepatikana kwa njia haramu! Waswiss walitaka Kabila
awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola bilioni nane za Kimarekani
Mobutu hakuzipata kihalali ndio waweze kuzirejesha. Zaire ilikadiriwa
kuwa na zaidi ya dola za Kimarekani bilioni thelathini katika Mabenki ya
nje ya nchi hiyo. Majibu ya aina aina hii ni majibu ‘standard’ ambayo
kila nchi inapewa. Hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao
walijibiwa hivi hivi. Hatimaye Serikali ya Marekani ikaamua kununua
taarifa hizo na kuwakamata wakwepaji kodi wao walioficha fedha Uswisi.
Hao ndio Waswiss ambao Serikali ya Tanzania inashabikia majibu yao. Bila
Aibu Mawaziri wetu wanayanukuu majibu ya Waswiss kama kasuku. Tunasahau
historia haraka sana. Tunakuwa kama mazezeta.
Tusiwe Taifa la mazezeta. Mabwege na mazezeta huimba kila
wanachoambiwa kuimba. Sasa Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji wa
Serikali ya Swiss badala ya kuchunguza utoroshaji wa fedha haramu na
kisha kutoa taarifa Bungeni. Naitaka Serikali ianze uchunguzi mara moja
kama namna ilivyoelekezwa na Bunge. Suala hili sio suala la kisiasa,
sasa ni Azimio la Bunge ambalo linahitaji kutekelezwa kikamilifu. Suala
hili sio suala la Zitto Kabwe tena, ni suala la Bunge, ni suala la
Wananchi. Wananchi hawataki uzezeta wa watu waliopewa dhamana ya
kutekeleza Azimio lao. Kama hawawezi wapishe watu wenye uwezo wa
kusimamia maslahi ya Watanzania kwa kuchukua hatua stahili za kuchunguza
utoroshaji mkubwa wa fedha za kigeni, ukwepaji mkubwa wa kodi na
ufisadi uliopelekea Watanzania kuficha mabilioni kwenye mabenki nje ya
Tanzania. Hatutakaa kimya mpaka tuone mwisho kamilifu wa suala hili.
Utekelezaji wa Azimio la Bunge itakuwa ni salamu tosha mafisadi na
watoroshaji wa fedha haramu kwamba hawana pa kujificha na Tanzania sio
Taifa la kuchezeachezea. Lazima tushinde vita hii. Anayeona hawezi
kutuongoza kuishinda atupishe mapema. Hatupaswi kuwa Taifa la Mazezeta.
Watanzania sio mabwege tena, Mwakyembe alipata kusema.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini.
No comments:
Post a Comment