RAIS wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila
ameikumbuka Tanzania na kusema kuwa harakati za kuikomboa nchi yao
walizifanya nchini humo kama walivyofanya baadhi ya marais wengine wa
Afrika.
Rais Kabila alisema hayo jana Ikulu mjini Kinshasa
wakati alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari wa Tanzania
walioko nchini Congo kwa ziara ya siku tano ya kikazi.
Alisema yeye binafsi amewahi kuishi maeneo mengi
ikiwa ni pamoja na Nairobi nchini Kenya, Kampala nchini Uganda na Dar es
Salaam nchini Tanzania.
“Tanzania ni nchi ambayo ilitukaribisha wakati
tukiwa katika harakati zetu kama ilivyofanya kwa Samora Machel, Joachim
Chissano na wengine,”alisema Rais Kabila.
Hata hivyo pamoja na kueleza hayo Rais Kabila
hakutaka kuelezea kama Serikali ya Tanzania iliwasaidia vipi kuhakikisha
wanaikomboa nchi ya Congo kutoka kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Mobutu
Seseko.
“Kuhusu kama tulisaidiwaje hilo ni jambo ambalo
siwezi kulizungumzia hapa, nikija Dar es Salaam ninaweza kuwaeleza na
hata kuwaonyesha niliishi maeneo gani katika jiji la Dar es
Salaam,”alisema Rais Kabila.
Alisema kitu muhimu ambacho anakumbuka kuhusu Tanzania ni kwamba ni nchi yenye amani na utulivu.
Akizungumzia mikakati mbalimbali ya Serikali yake
na changamoto katika kuijenga nchi ya Congo, Rais Kabila alisema hivi
sasa wameweza kuibadilisha nchi hiyo na kuwa nchi inayoweza kukalika kwa
amani isipokuwa eneo moja tu la Mashariki ambalo limekuwa na vita kila
wakati.
“Suala la vita Mashariki ni matatizo ambayo
tumeyarithi na kwamba yako kuanzia miaka ya 60 lakini vile vita vingine
tulivyokuwa navyo nchini viliisha mwaka 2009 , hivi sasa tunajitahidi
kuleta amani Mashariki ya Congo,”alisema Rais Kabila.
Alisema ukosefu wa amani katika eneo hilo
unasababishwa na nchi jirani hasa Rwanda hivyo wanajitahidi kuhakikisha
hilo lina kwisha kwa njia ya mazungumzo.
“Hivi sasa lengo letu kubwa ni kufikia amani ya
kudumu kwa kuzungumza. Sasa muda umefika kwani tunachotaka ni
amani,”alisema Rais Kabila.
Alisema amekutana na viongozi wote wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki(EAC), ili kuweza kuhakikisha amani katika eneo la
Mashariki ya Congo inapatikana kwa mazungumzo na si vinginevyo.
No comments:
Post a Comment