MATUMIZI ya noti mpya na za zamani katika mzunguko kwa karibu
miaka miwili sasa, yanatajwa kuwa kashfa nyingine kwa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT), baada ya ile ya wizi uliofanyika katika Akaunti ya
Madeni ya Nje, (EPA).
Baada ya BoT kuzindua noti mpya za Sh1,000, 2,000, 5,000 na 10,000 Januari 2011, Gavana Benno Ndullu alitangaza kuwa noti za zamani zenye thamani sawa na hizo, zingeondolewa kwenye mzunguko ndani ya kipindi cha miezi sita, ahadi ambayo mpaka sasa haijatekelezwa.
Akizungumzia hali hiyo mwanzoni mwa wiki, Gavana Ndullu alisema, hawezi kusema lini noti za zamani zitakwisha matumizi yake kwa kuwa hili litategemea kumalizika kwa noti hizo kwenye mzunguko.
Tangu noti mpya zilipoingia katika mzunguko, taifa limekuwa likitumia noti za aina mbili kwa pamoja, kitendo ambacho kimezua mjadala, huku baadhi ya watu wakieleza kuwa kinahatarisha uchumi wa taifa.
Watu wa kada mbalimbali waliozungumza na gazeti hili wameitupia lawama BoT, wakisema imeshindwa kuweka usimamizi mzuri wa fedha ama kwa makusudi au uzembe, hivyo kutoa fursa kwa watu wasio waaminifu kuingiza fedha chafu kwenye mzunguko.
“Biashara ya noti bandia inaonekana kama halali…, wanasema ukipeleka Sh100,000 unauziwa noti bandia za Sh200,000 namna ya kuzibadilisha utajua mwenyewe,” alieleza meneja wa benki moja mjini Moshi, ambaye hakutaka atajwe gazetini.
Kwa nyakati tofauti maofisa wengine wa benki kutoka mikoa ya Dare es Salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza na Kilimanjaro, walidokeza kuwa noti za zamani ni bora ikilinganishwa na noti mpya.
Mbali na kuchakaa haraka, maofisa hao wamesema noti mpya ni rahisi kughushiwa na maeneo salama ya kuzipeleka fedha hizo ni vijijini.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema kimsingi hakuna athari zozote kiuchumi kama nchi itaendelea kutumia noti mbili zenye thamani moja, lakini hii inatoa mwanya wa kusambaa noti bandia kwenye mzunguko wa fedha.
“Kama moja ya noti hizo zinaghushika kirahisi, watu wataghushi na kuziingiza kwenye mzunguko. Huu ni udhaifu wa Benki Kuu katika kusimamia suala hilo. Fedha hizo zinatakiwa zifike benki na zikienda huko, zisitolewe tena kwa wananchi,” alisema.
“Kuna uwezekano noti hizo kutokubalika kwenye baadhi ya maeneo,” alisema.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi katika Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Moris Oyuke pamoja na kusema kuwa kutumika kwa noti tofauti zenye thamani moja hakuna madhara kiuchumi, alisisitiza kuwa hali hiyo inapaswa kudhibitiwa.
“Kama BoT inapata Sh10,000 iliyochakaa na kuiharibu, kisha kutoa Sh10,000 mpya, hapo hakuna madhara. Tatizo linakuja kama BoT itaharibu kiasi kidogo cha fedha na kuingiza katika mzunguko fedha nyingi zaidi, hii italeta mfumko wa bei,” alisema.
Mkuu wa Idara ya Fedha katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Esther Ishengoma alisema kuwa kuwepo kwa noti mbili katika mzunguko kunaleta mkanganyiko katika jamii.
Dk Ishengoma alibainisha kuwa noti za zamani ni ubora zaidi ya noti mpya na inawezekana Serikali imeliona hilo ndiyo maana inashindwa kuziondoa katika mzunguko.
No comments:
Post a Comment