Friday, November 16, 2012

Dk Bilali: Sijaficha mabilioni Uswisi,wengi waanza kuhaha na kujitetea

MAKAMU wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilali, amesema yeye siyo miongoni mwa vigogo wa Serikali wanaodaiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi katika sakata lililoibuliwa hivi karibuni na  Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
 
Dk Bilali alitoa kauli hiyo jana kwenye mhadhara wa 13 wa kumbukumbu ya kumuenzi aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Hayati Edward Moringe Sokoine, akijibu swali la mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Jonson Robert.
Katika swali lake hilo, Robert alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kushughulikia tuhuma za mabilioni ya fedha yaliyofichwa nchini Uswisi, kama ilivyowasiliswa bungeni na Zitto katika hoja yake binafsi.
Robert alisema ukimya wa Serikali katika suala hilo na kutochukua hatua za haraka kunawafanya waamini kwamba huenda hata viongozi wa juu wanahusika na ufichaji wa fedha hizo.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais, tumesikia kuhusu umuhimu wa Sokoine katika kulinda rasilimali za taifa na kupambana na wahujumu uchumi, sasa je Serikali imechukua hatua gani dhidi ya watu wanaodaiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi?,” alihoji mwanafunzi huyo katika sehemu ya swali lake.
Akijibu swali hilo, Dk Bilali mbali na kueleza hatua ambazo Serikali imezichukua alisema kuwa yeye si miongoni mwa watu wanaotuhumiwa kuficha fedha hizo nchini Uswisi.
Dk Bilali alisema suala hilo limeshafikishwa serikalini na tayari hatua kadhaa za kisheria zimeanza kuchukuliwa na kama endapo kuna watu watabainika kuhusika na ufisadi huo, sheria itachukua mkondo wake.
"Serikali ya Mheshimiwa, Dk Jakaya Mrisho Kikwete iko tayari kulishughulikia suala hilo kama watu hao wapo, tusaidieni kuwapata watu hao," alisema Dk Bilali.
Awali tuhuma za kuwapo kwa vigogo waliochota mabilioni na kwenda kuyaficha katika benki mbalimbali, zilitolewa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama hoja binafsi na mbunge huyo, kisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuahidi Bunge hilo kuwa Serikali italifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na mbunge huyo.
Chimbuko la hoja
Mapema mwaka huu, baadhi ya vyombo vya habari likiwamo gazeti hili, vilifichua kuwapo kwa fedha zilizofichwa nchini Uswisi na baadaye ilibainika kwamba fedha hizo ni mali ya Watanzania 27 wakiwamo wanasiasa na wafanyabiashara.
Gazeti hili pia lilibaini kwamba mmoja wa walioficha fedha hizo anamiliki Dola za Marekani milioni 56 (sawa na Sh89.6 bilioni).
Katika uchunguzi wake, Mwananchi limebaini pia kwamba kiasi cha fedha kilichothibitishwa kumilikiwa na Watanzania hao ni jumla ya Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300 bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1600 kwa Dola ya Marekani.

No comments:

Post a Comment