Tuesday, November 20, 2012

Eckernforde baada ya kuzuiwa waomba usajili

BARAZA la Famasia nchini, limekizuia Chuo Kikuu cha Eckernforde cha Tanga (ETU) kutoa kozi ya sayansi ya afya kwa sababu hakijasajiliwa kisheria kuendesha mafunzo hayo.
Limetoa zuio hilo kupitia tangazo lilitoa wiki iliyopita katika vyombo vya habari na Msajili wa Baraza la Famasia, kwa madai kwamba hakijaidhinishwa wala kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Famasi ya mwaka 2011.

Kwa mujibu wa tangazo hilo,Oktoba mwaka huu ETU ilitoa tangazo kwenye vyombo vya habari la wito wa maombi ya kujiunga na kozi za cheti na stashahada za Sayansi za Afya kwa mwaka wa masomo wa 2012/13.

“Kwa kuzingatia sheria ya famasi 2011, baraza linapenda kutoa taarifa kwa umma kuwa ETU hakijaidhinishwa wala kusajiliwa na baraza, hivyo hakikubaliki kutoa mafunzo ya aina yoyote ile katika taaluma ya dawa (Certificate, Diploma or Bachelor in Pharmaceutical Sciences),” inasema sehemu ya tangazo hilo.

Tangazo hilo linaeleza kuwa, hata mitalaa yake ya kufundishia haijaidhinishwa wala kusajiliwa na baraza hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ETU, Remigius Tarimo alikiri kupokea barua  kutoka baraza la famasia kuzuiwa kuendesha kozi hiyo, lakini akadai mchakato wa kuomba usajili umeanza.

Tarimo alisema zuio hilo lilitolewa baada ya chuo kutoa tangazo la wito wa maombi ya kujiunga na kozi za cheti na stashahada za sayansi za afya kwa mwaka wa 2012/13.
“Nakiri kwamba kulitokea sintofahamu kwa wataalamu wa chuo chetu, walidhani wametimiza masharti yote kumbe hawakuwa wametimiza masharti ya Baraza la Famasia,” alisema Tarimo.

Alisema tayari maofisa kutoka Baraza la Famasia wamewasili chuoni hapo mwishoni mwa wiki iliyopita kufanya ukaguzi na kujiridhisha.

Alisema anategemea mchakato wa kukamilisha masharti ya baraza la famasia utakamilishwa mapema iwezekanavyo bila kuwaathiri wale waliokuwa wamewasilisha maombi ya kujiunga na kozi hiyo.

No comments:

Post a Comment