MBUNGE wa wa Jimbo la Kawe(Chadema), Halima Mdee,amewataka wakazi wa
mkoa wa Manyara kujiandaa kutwaa ardhi na mashamba ya wawekezaji ambayo
hayajaendelezwa kuanzia mwakani.
Akizungumza katika mkutano wa
hadhara katika uwanja wa michezo Babati, Mdee alisema haiwezekani ardhi
yote yenye rutuba nchini kumilikishwa wageni wakati Watanzania
wakitaabika.
Mdee ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema wawekezaji hao wamemilikishwa
ardhi yenye rutuba kwa kulipa Sh 2000 tu kwa heka kwa mwaka, wakati wao
wanatumia mashamba hayo hayo kuwakodishia Watanzania kwa Sh 100,000 kwa
mwaka kwa heka.
"Kama mlivyosikia bunge lililopita tumewasha moto
bungeni juu ya ardhi na wabunge wa CCM wametuunga mkono, sasa
tunasubiri bunge la mwezi wa nne, mwakani kisipoeleweka kaeni mkao wa
kula kutwaa mashamba"alisema Mdee.
Alisema tayari pia Waziri
wa Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk Mary Nagu alitoa kauli bungeni ya
wawekezaji kupewa mwaka mmoja kuendeleza mashamba la sivyo watapokonywa.
Mdee
alisema Watanzania hawawezi kugeuzwa watumwa kwenye ardhi yao na sasa
wamechoka ndio sababu Chadema, inataka taarifa ya bungeni juu ya ardhi
yote iliyopo nchini, iliyotolewa kwa wawekezaji na iliyobaki.
"Hapa
Babati kuna ardhi zaidi ya hekari 250,000 inamilikiwa na wawekezaji
Wazungu na Wahindi ambao hawaitumii ardhi yote badala yake wanakodisha
kwa Watanzania"alisema Mdee.
Akizungumzia Halmashauri ya Babati,
alieleza kusikitishwa na wakazi wa Babati kuwachagua madiwani wote wa
CCM na mbunge wa CCM, ambao wameshindwa kuwatetea.
"Mbunge wenu
kila siku yupo jimboni kwangu Mbezi Jijini Dar es Salaam, kwani ndiko
anaishi muda mrefu, mlimuaacha Paulina Gekur sasa mnajuta"alisema Mdee.
Hata
hivyo, alisema yaliyopita si ndwele wagange yajayo katika kuhakikisha
wanachagua madiwani na wagombea wa Chadema katika chaguzi zijazo.
Awali
Wabunge wa Viti Maalum , Paulina Gekur Rose Kamili na Cesilia Pareso,
waliwataka wakazi wa Jimbo la Babati, kubadilika sasa na kutambua kuwa
ukombozi wao upo Chadema.
Gekur alieleza kazi aliyofanya katika
Halmashauri ya Babati, ikiwepo kuzuia ushuru holela wa machinjio, kuzuia
wamachinga kuhamishwa bila utaratibu na kufichua ufisadi katika
halmashauri.
"Ndugu zangu japo kuwa mimi nipo mmoja tu katika
baraza la madiwani nadhani mnajua kazi kubwa ambayo nafanya
kuwatetea"alisema Gekur.
Nao Pareso na Kamili walisema viongozi
wa CCM wameshindwa kuwadhibiti watendaji wa serikali wasiwahujumu
wananchi na suluhu ya maisha bora kwa wananchi ni kuchaguwa Chadema
katika nafasi mbali mbali.
No comments:
Post a Comment