RAIS Jakaya Kikwete amesema mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati
ya Tanzania na Malawi bado unajadiliwa na nchi hizo mbili, hivyo hakuna
haja ya mataifa mengine kuingilia.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana mkoani Arusha alipokuwa akifungua mkutano wa tatu wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo Rais Kikwete alizindua mkakati wa pili wa chombo kinachoshughulikia masuala ya ulinzi, siasa na usalama katika nchi za Sadc ambazo ni Tanzania, Msumbiji, Zambia, Malawi, Botswana, Afrika Kusini, Namibia, Lesotho, Zimbabwe, Swaziland na Angola.
“Tanzania na Malawi bado tunazungumza kuhusu suala hilo na bado halijatushinda,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema vyombo mbalimbali ikiwamo Sadc, vina wajibu wa msingi wa kuingilia suala hilo, lakini kwa kuwa Tanzania na Malawi bado wako kwenye meza ya mazungumzo, sasa siyo wakati mwafaka.
“Malawi na Tanzania bado tuko kwenye mazungumzo, tusingependa nchi au mtu yeyote aingilie kati suala hilo kwa namna yoyote ile, ” alisisitiza Rais Kikwete.
Rais Kikwete alikwenda mbali zaidi na kueleza kuwa suala hilo liko mikononi mwa nchi hizo mbili, hivyo ni vyema likaachwa kwanza mazungumzo yaendelee kabla ya kuingiza nguvu ya ziada.
Alisema kwamba Tanzania na Malawi bado zinaangalia ni namna gani ya kuutatua mgogoro huo bila athari kwa pande mbili na kuomba mazungumzo ya amani yaendelee kuchukua mkondo wake.
Kuhusu mkakati wa pili wa chombo kinachoshughulikia masuala ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi za Sadc, Rais Kikwete alisema chombo hicho kiko imara na kimejidhatiti kuyasimamia masuala hayo kwa umakini zaidi.
Alisema kwa mara ya kwanza mkakati huo ulizinduliwa mwaka 2004, lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, masuala ya uharamia na biashara ya usafirishaji wa binadamu miongoni mwa nchi za Sadc, ndiyo maana mkakati wa pili umezinduliwa mwaka huu.
Katibu Mtendaji wa Sadc, Thomas Salomao aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba kuna sera mbalimbali zilizotungwa ndani ya chombo hicho kupambana na rushwa, dawa za kulevya na sera za masuala ya ulinzi na usalama.
Kauli ya Rais Kikwete kuhusu mgogoro wa mpaka katika Ziwa Nyasa, imekuja siku nne baada ya ujumbe wa Tanzania na Malawi kukutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumzia mgogoro huo.
Katika mkutano huo wa Dar es Salaam, nchi hizo mbili zilikubaliana kuwaita marais wastaafu wa nchi za ukanda wa Sadc kusaidia kumaliza mgogoro huo kwa amani.
Akizungumza baada ya mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe hivi karibuni alisema: “Tumekubaliana kutokubaliana, hivyo tulifikiana kuwatumia wakuu wastaafu wa Mataifa ya Sadc kusaidia kutatua mgogoro huu.”
Membe alitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari katika mkutano uliomshirikisha pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Ephraim Chiume.
No comments:
Post a Comment