Kasi ya walioanguka kwenye zoezi la kura
za maoni ndani ya CCM kukihama chama hicho imeendelea baada ya aliyekuwa
mgombea ubunge Jimbo la Same Mashariki, mkoani Kilimanjaro, Naghenjwa
Kaboyoka, kujiengua na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema).
Baada ya kutangaza kuhama CCM, jana
Kaboyoka, alichukua fomu ya kuwania ubunge Jimbo la Same Mashariki kwa
Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, Juma Iddi.
Akizungumzi uamuzi wake wa kujiengua CCM, Kaboyoka alisema ni kutokana na
utaratibu mbovu na haki kutotendeka
katika zoezi zima la kura za maoni ambapo alishika nafasi ya pili baada
ya Anne Kilango Malecela, ambaye ameteuliwa na CCM. Alisema misingi ya
uchaguzi haikufuatwa na kwamba aliandika barua ya malalamiko kwa katibu
wa CCM wilaya, mkoa na Taifa, lakini hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa, huku wakimbeba Kilango bila kuchunguza kasoro
zilizolalamikiwa.
“Mfano, orodha ya wapiga kura haikuwepo
na baadhi ya makatibu wa kata walikuwa na karatasi za kupigia kura
ambazo zimeandikwa jina la
Kilango na ambazo baadhi zilikamatwa na
kuwasilishwa kwa viongozi wa ngazi za juu, lakini hawakuchukua hatua,
watu wasio wanachama walipewa kadi na kupiga kura,” alisema.
Alisema mamluki wengi wasio wanachama
walipewa kadi za kupigia kura na hata wale ambao hawakuandikishwa katika
daftari la wapiga kura la chama na wasio na kadi waliruhusiwa kupiga
kura, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
“Nimeamua kwenda chama cha upinzani
ambacho ni Chadema, nimejiridhisha kuwa kina sera nzuri na ambazo
nimezipenda na zinazowafaa wananchi wa jimbo langu, na pia baada ya
wananchi kuona utaratibu huo mbovu walikasirishwa na kuniomba niende
chama kingine ili wanichague,” alisema Kaboyoka.
Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro,
Basil Lema, alithibitisha Kaboyoka kujiunga na chama hicho na kuchukua
fomu ya kuwania ubunge katika jimbo hilo na kwamba wamempokea kwa furaha
na matumaini makubwa.
“Tumefurahi, tumepata mpambanaji
mwenzetu, kwa muda mrefu tangu mwaka 2000 amekuwa akiambiwa ndani ya
chama hicho asubiri, kasubiri vipindi vitatu huku wakati hausubiri,”
alisema na kuongeza: “Hivyo ni vyema awatumikie wananchi sasa iwapo
watampa nafasi hiyo.”
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Ali Idi, alithibitisha kutoa fomu ya kugombea ubunge kwa Kaboyoka.
No comments:
Post a Comment