CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeunda Sekretarieti mpya katika uongozi
wake, huku wakongwe wakirejeshwa, akiwamo Abdulrahaman Kinana
aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Kinana mwanasiasa
wa siku nyingi ambaye amekitumikia chama hicho kwa miaka 25, anachukua
nafasi ya mtangulizi wake, Wilson Mukama ambaye ameng’olewa katika
nafasi hiyo na kuweka rekodi ya kuwa Katibu Mkuu aliyekaa kwa muda mfupi
wa miaka miwili tu.
Wengine katika Sekretarieti iliyotangazwa
jana na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ni pamoja na Mbunge wa
Kuteuliwa, Zakhia Meghji, Mbunge wa Uzini, Mohamed Seif Khatibu na Naibu
Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha- Rose Migiro.
Akitangaza
safu hiyo mpya ya uongozi baada ya kumalizika kikao cha Halmashauri
Kuu (Nec) ya chama hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa White House
jana, Rais Kikwete aliwataja wengine aliowateua kuwa ni Vuai Ali Vuai
ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.
Alisema Mbunge wa Iramba
Magharibi, Mwigulu Nchemba amepandishwa kutoka Katibu Uchumi na Fedha na
kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na
Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati.
Alisema Meghji
atakuwa Katibu wa Uchumi na Fedha akichukua nafasi iliyokuwa
ikishikiliwa na Nchemba, wakati Khatib ameteuliwa kuwa katibu wa
Oganaizesheni ya chama hicho, nafasi ambayo katika Sekretarieti
iliyopita ilikuwa ikishikiliwa na Asha Abdallah Juma.
Dk Migiro
ameteuliwa kuwa Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, nafasi ambayo
ilikuwa ikishikiliwa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba.
Kwa mujibu wa kanuni za CCM,
mawaziri hawaruhusiwi kuwa watendaji katika sekretarieti ya chama, hivyo
Makamba asingeweza kuteuliwa tena isipokuwa kwa sababu maalumu.
Dk
Migiro kama ilivyo kwa Meghji aliwahi kushika wadhifa huo kabla ya
kuteuliwa kwenda Umoja wa Mataifa. Rais Kikwete alisema chama hicho
kimemteua Nape Nnauye kuendelea na wadhifa wake wa Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa chama.
Alisema ameshindwa kuteua wajumbe wa Kamati Kuu
kwa sababu wajumbe wa Nec bado ni wapya na kwamba apewe muda wa
kuangalia atakaowateua.
“Uteuzi wa Kamati Kuu, utafanyika
baadaye kwa sababu Nec hii ina watu wazuri na wapya, hivyo nipeni muda
niangalie nani nimteue kuingia katika Kamati Kuu,” alisema.
Walioachwa
Mukama aliyechukua nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM 2010, amepewa jukumu la kusimamia uanzishwaji wa chuo cha chama hicho.
Katika
uongozi wake, kiongozi huyo amekuwa akilalamikiwa na makada wa CCM
ambao wamekuwa hawaridhishwi na utendaji wake tangu alipoteuliwa, hasa
kuhusu utekelezaji wa mpango wa kujivua gamba ambao ulilenga kuwang’oa
watuhumiwa wa ufisadi.
Alitikiswa na siasa za makundi ambayo
yamekuwa yakipata nguvu kila kukicha, kutokana na kujipanga kuwania
urais wa 2015 kupitia CCM, na katika Uchaguzi Mkuu wa chama hicho,
alionekana kushindwa kukimudu chama kutokana na kushamiri kwa rushwa.
Mukama akizungumzia uteuzi wa kuongoza uanzishwaji wa chuo cha CCM alisema amefurahi kufanya kazi hiyo.
Alisema: “Nimefurahi sana, sina wasiwasi na majukumu mapya ambayo nimepewa, nitayamudu.”
Chiligati kwa upande wake anaondoka katika chama hicho baada ya kudumu kwa muda mrefu akiwa mjumbe wa Sekretarieti.
Awali
alikuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi na baadaye alipandishwa wadhifa na
kuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), nafasi iliyompa misukosuko hasa katika
kipindi ambacho CCM kilijaribu kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa
ufisadi.
Kwa upande wake, Asha Abdallah Juma, yeye ameachwa
kutokana na umri, hali ambayo imekuwa ikimfanya ashindwe kushiriki
kikamilifu katika harakati za kisiasa ndani ya CCM.
Kada huyo
wakati wa uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki mwezi Aprili mwaka huu,
alikuwa akitembelea fimbo na hakuwa na uwezo wa kusimama jukwaani kwa
muda mrefu.
Kikosi cha 2015
Makada wapya walioteuliwa
wanaungana na mkongwe mwingine, Makamu Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula
aliyerejeshwa katika uongozi wa juu wa chama, baada ya kuwa nje kwa
miaka mingi.
Mangula aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM wakati wa
uongozi wa Benjamin Mkapa alipata nafasi hiyo baada ya kukosa nafasi ya
kuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Iringa katika uchaguzi uliopita.
Baada ya kukosa nafasi hiyo aliendelea na shughuli za kilimo mkoani
humo.
Mangula kama alivyo Kinana wanatajwa kuwa watu makini na
kuwepo kwao katika nafasi za juu za uongozi wa CCM ni ishara kwamba
huenda chama hicho kimeamua kujipanga ipasavyo kwa ajili ya Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Mangula ni mmoja wa makada wa CCM walioitwa kuokoa
jahazi la chama hicho lisizame katika uchaguzi mdogo wa Ubunge katika
Jimbo la Igunga, ambako anatajwa kuwa alisaidia kuwabaini hata makada
ambao walikuwa wakitoa taarifa za uongo kuhusu uchaguzi huo.
Kinana
kama alivyo Mangula, amejizolea sifa ya kuwa kiongozi mkuu wa kampeni
za CCM tangu kuanza kwa siasa za vyama vingi nchini 1995, na tangu
wakati huo chama hicho hakijawahi kushindwa.
Siku chache
zilizopita alitangaza rasmi kustaafu siasa ndani ya CCM, hatua ambayo
iliwashtua sana makada wa chama hicho wakiwamo vigogo ambao tayari
walikuwa wameanza kumshawishi kukubali uteuzi wa nafasi ya Katibu Mkuu.
Habari
kutoka ndani ya CCM zinasema, kulikuwa na kazi kubwa ya kumshawishi
kukubali wadhifa huo na kwamba alitoa masharti magumu ambayo vigogo wa
chama hicho walilazimika kuyakubali ili “kukinusuru chama”.
Kauli za wateule
Akizungumzia kuteuliwa kwake, Kinana alisema ameupokea kwa furaha uteuzi huo ingawa ni dhamana nzito kuibeba.
Hata hivyo, alisema atajitahidi kadiri ya uwezo wake kumsaidia Mwenyekiti wa chama hicho kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM.
Kinana
alisema ingawa hivi karibuni alitangaza kustaafu uongozi ndani ya chama
hicho, lakini aliombwa na Rais Kikwete amsaidie, hivyo asingeweza
kukataa.
Alisema uamuzi wa kustaafu uongozi ulikuwa uamuzi wake binafsi baada ya kukaa katika uongozi wa chama kwa miaka 25.
Kinana alisema aliona ni vyema kukaa pembeni ili watu wengine ndani ya chama hivyo hususan vijana kuchukua nafasi za uongozi.
Kuhusu
uadilifu ndani ya chama hicho, alisema atatekeleza uamuzi wote wa vikao
na kwamba watautengenezea programu ya utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Meghji alisema amefurahi kuteuliwa katika nafasi hiyo ambayo inamwezesha kukitumikia chama tena.
Alisema
nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha wa chama ina changamoto nyingi hasa
kwa wakati huu ambapo chama hicho, kimeamua kujitegemea kiuchumi.
Hata hivyo, alisema anaamini kuwa atashirikiana na viongozi na wanachama wengine ili kufanikiwa kwa mipango hiyo ya chama.
“Naamini kuwa tutafanikiwa kufikia lengo hilo la chama kwa sababu tutashirikiana wote,” alisema.
Naye Dk Migiro alisema ameupokea uteuzi huo kwa furaha, kwa sababu ni kazi ya kukijenga chama chao.
Alisema kwake yeye ni heshima kubwa kupewa majukumu hayo ya kuitumikia nchi yake kupitia CCM.
“Ni heshima kubwa kupewa majukumu haya ya kuitumikia nchi yangu,” alisema.
Naye Mwingulu alisema ameufurahia uteuzi huo kwa sababu hakutarajia kuwa katika timu hiyo mpya.
Alisema amefurahishwa kupangwa katika timu mpya ya uongozi wa chama hicho ambayo anaamini ni ya ushindi.
“Nimepokea uteuzi, kwa mshtuko mkubwa na furaha , nimefurahishwa na timu mpya ambayo nimo ndani yake,” alisema.
No comments:
Post a Comment