Saturday, November 17, 2012

WAZIRI wa zamani wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Jackson Makwetta amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam jana.

Taarifa zilizopatikana jana na kuthibitishwa na mtoto wa marehemu, Tumwanuke Makwetta zilisema kuwa marehemu alifariki jana jioni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu.
Kabla ya kuhamishiwa Muhimbili, mwanasiasa huyo mkongwe nchini, alifikishwa Hospitali ya Lugalo wiki iliyopita  baada ya hali yake kuwa mbaya kutokana na maradhi ya moyo.
Mtoto wa marehemu, Tumwanuke Makwetta  aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa taarifa zaidi kuhusu msiba wa mzee wao zitatolewa baadaye.
“Kwa sasa siwezi kusema lolote kwa sababu ndiyo tunatoka hospitali kuelekea nyumbani, taarifa zaidi nitakujulisha baadaye,” alisema.
Mtoto wa marehemu alisema kuwa baba yao alifariki  jana jioni walipokwenda kumjulia hali.
Makwetta alianza kuugua akiwa nyumbani kwake Njombe na akapelekwa kutibiwa katika Hospitali ya Consolata ya Ikonda, wilayani Makete na baadaye wiki iliyopita alihamishiwa katika Hospitali ya Lugalo jijini Dar es Salaam baada ya kuzidiwa.
Muda mfupi kabla ya kifo chake, Rais Jakaya Kikwete alifika hospitalini hapo kumjulia hali.
Gazeti hili lililokuwa hospitalini hapo lilishuhudia msafara wa Rais ukifika hospitalini hapo na kuingia wodini na baadaye kuondoka.
Rais Kikwete alitumia fursa hiyo pia kuwapa pole wagonjwa wengine waliokuwa wakihudumiwa hospitalini hapo.
Wasifu
Alizaliwa Juni 15, 1943. Alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 1976-1980, mwaka 1982-83 alikuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Makwetta pia aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo na Chakula mwaka 1983-1987, alibadilishwa wizara na kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mwaka 1987-1989.
Marehemu alishika wadhifa wa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi mwaka mmoja kuanzia 1989-1990 na baadaye alihamishiwa Wizara ya Kilimo na Chakula mwaka 1991-1992.
Pia amewahi kuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu mwaka 1995-1998.
Makwetta amekuwa Mbunge wa Jimbo la Njombe Kaskazini tangu 1975 hadi 2005, alipoenguliwa katika kura za maoni na aliyekuwa mgombea mpya wa CCM, Deo Sanga.
Pia marehemu ni miongoni mwa mawaziri walioshika nyadhifa za uongozi katika Serikali ya Muungano katika awamu tatu; Awamu ya Kwanza ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Awamu ya Pili ya Ali Hassan Mwinyi na Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa.

No comments:

Post a Comment