Nimeamua kuchukua hatua ya kuiweka hadharani ripoti hii ya SIRI ya ndani ya Shirika la Umeme (TANESCO) ya maoni ya kisheria juu ya ukaguzi maalum uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi niliyoitoa tarehe 1 Novemba 2012.
Kwa mujibu wa nyaraka hii ni wazi aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Umeme (TANESCO) William Mhando amefanya makosa mengi
yanayohitaji hatua za ziada za kisheria ikiwemo ya mgongano wa maslahi,
utovu wa uaminifu, kushindwa kutangaza maslahi na matumizi mabaya ya
ofisi; matendo ambayo ni ya kifisadi.
Makosa hayo na mengine ni kinyume cha sheria mbalimbali za nchi ikiwemo
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria ya Ajira na Mahusiano
Kazini, Sheria ya Ununuzi wa Umma na sheria nyingine.
Hivyo, kwa kuwa Bodi imekataa kuwa haitachukua hatua za zaidi za
kisheria juu yake natoa kauli ya ziada kwamba mamlaka zingine
zinazohusika zichambue Taarifa hii sanjari na Taarifa ya Mkaguzi wa
Hesabu za Serikali (CAG) na kuchukua hatua za kisheria zilizochini ya
mamlaka hizo.
Mamlaka hizo ni pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sekretariati
ya Maadili ya Umma zote kila moja kwa nafasi yake zichunguze ukiukwaji
wa sheria katika masuala yaliyo kwenye majukumu yao na kuchukua hatua za
ziada.
Aidha, wakati mamlaka na taasisi hizo zikiendelea kuchukua hatua za
kisheria naitaka kwa mara nyingine bodi ieleze hatua ilizochukua dhidi
ya watendaji wengine wa TANESCO walioshirikiana naye kwa namna moja au
nyingine na iwapo bodi hiyo haitachukua hatua za haraka, ukiondoa majina
ya maafisa watatu waliosimamishwa mpaka sasa nitataja majina ya ziada
ya maofisa wengine waliohusika na kutaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia
kati kwa mamlaka yake ya kikatiba na kuchukua hatua ikiwemo dhidi ya
bodi yenyewe.
Ikumbukwe kwamba kufuatia kufukuzwa kazi kwa Mhando kwa nafasi yangu ya
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini tarehe 1 Novemba 2012 nilitoa kauli
ya awali kwamba hatua hiyo pekee haitoshi bali Serikali irejee katika
hotuba niliyotoa tarehe 27 Julai 2012 bungeni kwa niaba ya kambi rasmi
ya upinzani na kuchukua hatua zaidi za kuwezesha Mhando na wenzake
kufikishwa mahakamani.
Aidha, pamoja na hatua za ziada nilitaka bodi ya TANESCO kueleza hatua
ilizochukua dhidi ya watendaji wengine wa TANESCO walioshirikiana naye
kwa namna moja au nyingine na iwapo bodi hiyo haitachukua hatua za
haraka niliahidi kuiweka hadharani taarifa ya kamati iliyoundwa na bodi
hiyo kuchambua taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
kueleza hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na Rais Jakaya Kikwete dhidi
ya Bodi yenyewe.
Kufuatia kauli yangu hiyo tarehe 3 na 7 Novemba 2012 Mwenyekiti wa Bodi
ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Jenerali Mstaafu
Robert Mboma alinukuliwa baadhi ya vyombo vya habari akisema kwamba
aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo William Mhando hawezi
kushitakiwa mahakamani kwa sababu kosa alilofanya la kuingia kwenye
mikataba yenye mgongano wa kimaslahi ni kosa la kiuadilifu.
Mwenyekiti wa Bodi ametaja kosa moja tu la mgongano wa kimaslahi wakati
ambapo yapo makosa mengine na naamini kauli yake imetokana na ushauri wa
kwenye kipengele cha 36 na 37 cha nyaraka niliyoambatanisha; maoni
ambayo bodi ilipaswa kuyachukulia kwa tahadhari na kutaka mamlaka na
vyombo vya uchunguzi kuendelea na hatua zao za ziada kuwezesha hatua za
kisheria kuchukuliwa.
Aidha alieleza kwamba kuhusu maofisa wengine watatu waliosimamishwa
sambamba na Mhando bodi yake inasubiri taarifa ya ukaguzi unaofanywa na
Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kubaini kama
wana makosa wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na kuahidi kwamba
uchunguzi dhidi yao ungekamilika ndani ya wiki moja na kueleza kuwa
hatma yao ingejulikana tarehe 16 Novemba 2012 ahadi ambayo mpaka leo
tarehe 23 Novemba 2012 haijaitekeleza.
Katika muktadha huo kwa kuwa suala hili tayari limeshatolewa kauli
kwenye vyombo vya habari kwa nyakati mbalimbali na Wizara ya Nishati na
Madini pamoja na TANESCO, mawasiliano ya kawaida ya kiofisi na kuendelea
kuficha taarifa za siri kama hii hakutalisaidia taifa kujinusuru kwa
haraka na ufisadi. Hivyo, kusambaza taarifa hii hadharani na kutaka
majibu ya wazi toka kwa mamlaka zote zinazohusika kutawezesha hatua za
haraka kuchukuliwa kwa maslahi ya umma.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb) Waziri Kivuli wa Nishati na Madini.
No comments:
Post a Comment