Emmanuel Okwi
Taarifa zilizothibitishwa jana, zimetaja
mchanganuo wa ofa iliyotolewa kwa nyota hao kuwa ni dola za Marekani
50,000 kwa ajili ya kumtwaa Okwi, dola 40,000 za kumsajili Ngassa na
beki wa kimataifa wa Rwanda, Mbuyu Twite ametengewa dau la dola 100,000;
hivyo jumla ya fedha zote kufikia dola 190,000 (Sh. Milioni 300).
Akizungumza na NIPASHE jana, Mkurugenzi wa
klabu ya African Lyon inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Rahim
Kangezi, alisema kuwa uongozi wa klabu yake ndiyo unaowataka wachezaji
hao na tayari wameshaanza mawasiliano kwa kuziandikia barua klabu za
Simba na Yanga kwa nia ya kujaribu kufanya nao biashara, lakini hadi
sasa bado hawajajibiwa.
Kangezi alisema kuwa klabu yao ambayo iko
katika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi, iko kutoa fedha
hizo ili kuwatwaa nyota hao kwa vile wanajua kuwa watawasaidia kutimiza
malengo yao.
"Tayari tumeshampa barua Kaburu (Geofrey-
Makamu Mwenyekiti wa Simba) ila wanaonekana hawataki kutupa ushirikiano…
kuna wadau tumewapata ambao ndiyo wanatoa fedha hizo," alisema Kangezi,
ambaye ndiye alifanikisha usajili wa kiungo Nizar Khalfan kwenda
kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada
kabla hajahamia Philadephia Union na baadaye kurejea nchini kuichezea
Yanga.
Kangezi aliongeza kwamba wadau wao ambao
ndiyo wanaoisaidia Lyon wanataka kuona timu hiyo inaendelea kushiriki
kwenye ligi ya Bara na ndiyo maana wameahidi kuisaidia fedha za kusajili
wachezaji zaidi watakaowaongezea nguvu kikosini na kutimiza lengo la
kuibakiza timu yao ligi kuu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence
Mwalusako, aliliambia gazeti hili kwamba hawako tayari kumuuza mchezaji
wao yeyote ikiwa wanunuzi hawajafikia vigezo vyao, ikiwa ni pamoja na
kutanguliza ofa ya maana ya walau dola za Marekani 200,000 (Sh. Milioni
315).
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga na
katibu mkuu wake wake, Evodius Mtawala hawakupatikana jana kuzungumzia
suala hilo huku Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage akishindwa
kulielezea baada ya kusema kuwa yeye na viongozi wengine wa klabu yake
wako katika kikao cha kamati ya utendaji.
Katika hatua nyingine, Kangezi alisema
kuwa licha ya kutokuwapo na muafaka kati yao na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), bado wadhamini wao (Zantel) wanaendelea kuwapa fedha na
wiki ijayo wachezaji wataanza mazoezi kujiandaa na mzunguko wa pili wa
ligi.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment