Monday, November 26, 2012

Chadema uongozi balaa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitafutia dawa migogoro inayotokana na baadhi ya makada wake kuonyesha nia ya kuwania urais na ubunge mwaka 2015, baada ya kuanzisha utaratibu maalumu wa wanachama wake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gageti  hili, mpango huo unakuja wakati Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe ametangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao, kitendo ambacho kiliwashtua vigogo wa chama hicho akiwamo mwasisi wake, Edwin Mtei.

Mara kadhaa Mtei amekuwa akimwonya Zitto kuwa kitendo chake cha kutangaza nia yake ya kugombea urais kitasababisha mzozo na mpasuko ndani ya chama hicho.

Mtei amekuwa akisema kuwa Zitto anatakiwa kuwaunganisha wanaChadema na siyo kuwagawa, au kuwavuruga na kwamba siyo shida kuonyesha hisia za kuwania urais, lakini tatizo ni kuwa hali hiyo inatengeneza mzozo mkubwa.

Mtei ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu (BOT) enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema wakati mwafaka ukiwadia, Chadema kitaamua ni nani mwenye sifa za kugombea urais akisema kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea mbalimbali wa uongozi.

Akizungumza wakati akijibu hoja mbalimbali katika mtandao wa Jamii Forum katikati ya wiki hii, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema viongozi wa chama hicho walikutana mjini Morogoro hivi karibuni na kutengeneza utaratibu wa watu kutangaza nia wanapotaka kugombea nafasi yoyote ya uongozi.

“Nadhani huu ni uamuzi mzuri wa chama maana watu wengine wana wasiwasi usio na msingi wowote kwamba kuwa na wagombea wengi kwenye chama ni kuvuruga chama,” alisema Zitto na kuongeza:

“Lakini watu haohao wanashangilia kweli wakiona demokrasia inavyotekelezwa kwenye nchi nyingine kama Marekani.”

Alisema kuwa tatizo la Watanzania wanapenda kuona demokrasia inatekelezwa, lakini wao wanaogopa kuitekeleza, hivyo mwongozo kwa wagombea ambao walipitisha Morogoro utasaidia sana.

“Uamuzi wa Morogoro kuhusu mwongozo kwa wagombea utatusaidia sana kuondoa mashaka kama haya,” alisema Zitto.

Mwananchi Jumapili lilipomuuliza Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika kuhusu jambo hilo  alionyesha kutofahamu lolote kuhusu utaratibu huo, wala ulipofanyika huo mkutano wa Morogoro.

“Mkutano upi wa Morogoro?” alihoji Mnyika. Alipoelezwa kuwa suala hilo lilizungumzwa na Zitto katika Mtandao wa Jamii Forum alisema: “Muulize kwanza Zitto akupe ufafanuzi ni kikao gani cha chama, pia juu ya huo utaratibu, akikueleza ndiyo urudi tena kwangu.”

Juhudi za kumpata Zitto kueleza kwa undani kuhusu utaratibu huo hazikuzaa matunda, kwani simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila majibu, baadaye kuzimwa kabisa.

Akizungumzia azma yake ya kuachana na ubunge kama alivyoahidi mwaka 2005 kuwa, atagombea vipindi viwili pekee Zitto, alisema kuwa aliwaambia wapigakura wake kwamba nia yake ni kuwa rais wa nchi.

“Nia yangu ni kupisha wengine nao wakimbize kijiti cha maendeleo ya jimbo letu na mkoa wetu,” alisema Zitto na kufafanua, “ Nimeshasema mara kwa mara kwamba ukiachana na siasa kazi ninayoipenda zaidi ni ualimu.”

Alisema kuwa akiachana na ubunge atakwenda kufundisha kwa kuwa anapenda kufanya tafiti, kusoma, kuandika na kufundisha.

“Hivi sasa tunaandaa mpango wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Ziwa Tanganyika (Lake Tanganyika) mkoani Kigoma, nitafurahi kama nitakuwa mmoja wa wahadhiri wa mwanzo wa chuo hiki,” alisema Zitto.

Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alisimama kugombea nafasi ya urais akishindana na Rais Jakaya Kikwete ambaye alikuwa akisimama kwa mara ya kwanza.

Mwaka 2010, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willbrod Slaa aligombea nafasi hiyo na kuibuka mshindi wa pili kwa kupata asilimia 26.34 nyuma ya Rais Kikwete ambaye alipata asilimia 61.17.

Hivi sasa tayari kumetokea maneno ya chinichini miongoni mwa wabunge waliopo madarakani wakiwatuhumu baadhi ya wanachama wa chama hicho ambao wameaanza kuingia katika majimbo yao kutaka kugombea viti hivyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Wabunge hao wanahoji kama wanachama hao wanaofanya hivyo wanataka kugombea ubunge katika uchaguzi ujao ili kukifanya chama kiongeze idadi ya wabunge bungeni, kwa nini wasiende kugombea katika majimbo ambayo hayana  wabunge wa chama hicho?

Vilevile, chama hicho kilipata msukosuko katika mchakato wa kupata wabunge wa Viti Maalumu katika uchaguzi uliopita na kulazimika kuweka vigezo ambavyo viliondoa manung’uniko hayo.

Baadhi ya vigezo hivyo ni elimu, mchango wa mgombea katika chama, wanawake waliogombea katika majimbo na uzoefu katika ubunge.

E & P


No comments:

Post a Comment