Friday, November 16, 2012

CCM wamhusisha Karume na Uamsho

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Aman Karume juzi usiku alizomewa na baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakimwita kwamba ni mmoja wa wanakundi la Uamsho.


Uamsho ni kundi ambalo katika siku za hivi karibuni limekuwa likihusishwa na vurugu ambazo zimekuwa zikitokea Tanzania Visiwani, ambazo zimesababisha watu kadhaa kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Rais Karume alikutana na zahama hiyo wakati akitoa hotuba ya kuwaaga wanaCCM baada ya kumaliza ngwe yake ya utumishi ndani ya chama hicho akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar.

Dalili za Rais Karume kuzomewa zilianza baada ya baadhi ya wajumbe kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi kuanza kutaja neno ‘Uamsho’ kila alipokuwa akizungumzia matatizo yaliyopo Zanzibar.

Hali ilikuwa mbaya zaidi pale alipokuwa akizungumzia vurugu za kidini ambazo ziliikumba Zanzibar hivi karibuni zikiongozwa na kikundi cha Uamsho.

Karume alisema kuwa kikundi cha Uamsho kina haki ya kutoa maoni yake kuhusu muungano, lakini hakipaswi kufanya vurugu kama ambavyo kimekuwa kikifanya.

Wakati akiendelea kuzungumzia suala hilo, kelele nyingi zilienea katoka kwa wajumbe wa mikoa ya Zanzibar ambao walikuwa wakipaza sauti, “ Uamsho huyo….Uamsho huyo… Uamsho huyo….”

Hali hiyo ilimfanya wakati mwingine kukatiza hotuba yake na kulazimisha kuwatuliza watu hao kwa kusema “CCM oyeee….CCM…..oyeee…Mapinduziii….”
Hata hivyo, baada ya kelele hizo kuendelea Karume alionekana kuhamaki na kuwaambia wajumbe hao kwamba amechoka kusikia akiitwa jina hilo la Uamsho.

“Nimechoka kusikia naitwa jina hilo ati,” alisema Karume na kuongeza:
“Hivi wengine wana vichwa vya samaki kwa nini mnapiga kelele wakati mimi ninapozungumza, si mniache nizungumze mambo ambayo ni muhimu zaidi kwa masilahi ya chama chetu.”

Hata hivyo, licha ya kutafuta namna ya kuwatuliza wanachama hao kwa maneno mengi na historia ya maisha yake tangu alipojiunga na Chama cha ASP mwaka 1970, bado hakukuwa na utulivu na safari hii kelele zilianza kwa pande zote za wajumbe.

Kwa upande wa wajumbe wa Bara, baadhi yao walikuwa wakipiga kelele za kumtaka kumaliza hotuba yake ambayo walisema ilishachukua muda mrefu huku wakisema hakuna cha ajabu alichokuwa akizungumza.

Mara baada ya kumaliza hotuba yake, Karume alihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Deutche Welle ya Ujerumani, na alisisitiza kuwa Uamsho wana haki ya kutoa maoni yao kuhusu muungano, lakini hawaruhusiwi kuvunja sheria.

Aliwataka wanachama wa kikundi hicho kujenga hoja, kwani alisema wengine wana hoja za msingi, lakini wasitumie vitisho.

Karume alistaafu uongozi wa CCM katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Tanzania Visiwani) na nafasi yake ilichukuliwa na Rais wa sasa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein.

Tofauti na utamaduni ambao CCM kimeujenga kwa viongozi wake wakuu, Karume aliendelea kuwa makamu mwenyekiti hata baada ya kustaafu urais wa Zanzibar, hivyo kumlazimisha Dk Shein kusubiri hadi juzi kuchukua nafasi hiyo.

Kwa kawaida, viongozi wa ngazi ya Rais wa Muungano na Zanzibar, baada ya kuondoka katika nafasi zao za uongozi wa nchi, pia huachia madaraka ndani ya chama na kumwachia Rais mpya.
chanzo-Mwananchi

No comments:

Post a Comment