ABIRIA wanaotumia usafiri wa treni Dar, juzi walimtoa kijasho Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, alipokwenda kuwasimamia abiria hao
wapande kwa foleni kwenye treni inayotoka Stesheni kwenda Ubungo
Maziwa.Dk Mwakyembe aliwasili eneo hilo kati ya saa tisa alasiri na saa
kumi na moja jioni kushuhudia usafiri huo unavyoendelea, ambapo
alikutana na kadhia mbalimbali kwenye huduma hiyo mpya jijini.
Alitumia
kipaza sauti kutoa maagizo kwa abiria kusimama kwenye foleni, lakini
jitihada zake zilichukua muda kueleweka kwani kadri alivyokuwa
akitangaza ndivyo abiria hao walivyomzonga.
“Nasema simameni
kwenye foleni, kama mtu hatasimama kwenye foleni hatapanda” alisema Dk
Mwakyembe mara kwa mara lakini abiria badala ya kufanya kile
alichowaagiza walikuwa wakimsonga wengine kwa kutaka kumwona, wengine
wakitaka kusikia anachosema.
Pengine ujio wa Waziri huyo mwenye
dhamana ya usafiri ulikuwa kivutio kituoni hapo kwani alipotoa maagizo
kwenye behewa moja na kuhamia behewa jingine watu walikuwa wakimfuata
hali iliyosababisha usumbufu.
“Waziri sisi tumekuja mapema hapa
na tulifuata utaratibu lakini kuna watu wengine wanaharibu foleni”
alisema abiria mmoja, lakini hakusikika kutokana na kelele nyingi.
Huku
wakimwonyesha tiketi kuhalalisha uwepo wao kwenye foleni, Dk Mwakyembe
ambaye alikuwa amesimama kwenye mlango wa kuingilia alizidi kusisitiza
abiria kujipanga kwenye foleni lakini ni wachache waliomuelewa.
Baadaye
kidogo alipozungumza na Maofisa wa Kampuni ya Reli(TRL) Dk Mwakyembe
aliwaambia; “Tukishindwa kujiwekea misingi sasa hivi huko mbele utakuwa
ugonjwa na maradhi yasiyotibika.”
“Nimetoka bungeni kwa sababu
hii nije nione kinachoendelea” alisema Waziri Mwakyembe ambaye jana
aliacha kikao kinachoendela mjini Dodoma kuja Dar es Salaam kwa sababu
hiyo.
“ Bora wasafiri abiria 20 wenye nidhamu kuliko kupeleka
abiria 300 hovyo hovyo” alisema Dk Mwakyembe ambaye alifuatana na Katibu
Mkuu wa wizara hiyo Mhandisi Omar Chambo.
Katika hatua nyingine
MAMLAKA ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), imeelemewa na wingi wa
abiria wanaotumia usafiri huo jijini Dar es Salaam kutokana na mwitikio
mkubwa wa wananchi katika kutumia huduma hiyo.
Hayo yameelezwa na Ofisa Usalama wa Mamlaka hiyo, Hanya Mbawala, alipokuwa akizungumza na Mwananchi ofisini kwake jana .
“Abiria
wanaotumia treni ni wengi tofauti na mategemeo yetu, hii inatupa
changamoto ya kuongeza idadi ya mabehewa ili kuweza kukidhi
mahitaji”alisema Mbawala.
Mbawala alieleza kuwa Tazara ina mpango
wa kuongeza idadi ya mabehewa saba ifikapo Machi mwakani ili kupunguza
msongamano wa abiria.
“Tunatengeneza mabehewa mengine saba ambayo
mpaka Machi mwakani yatakuwa yamekamilika, tutakuwa tukiongeza behewa
moja kila linapo kamilika” alisema.
Aliongeza kuwa wanatarajia
kuimarisha ulinzi ili kudhibiti abiria wasio waaminifu katika kulipa
nauli baada ya kutumia usafiri huo sambamba na kurahisisha upatikanaji
wa tiketi kwa kila abiria.
Tangu kuanza kwa usafiri wa treni
jijini Dar es Salaam wadau wa usafiri huo wameeleza kuwa upatikanaji wa
tiketi imekuwa ni changamoto jambo ambalo linaweza likapunguza mapato
kwa mamlaka husika.
Akilizungumzia suala hilo Mbawala alisema
kuwa tiketi zinazo tumika zinazalishwa na kampuni ya Selcom ila
wanatarajia kuwa na kikao nao kulizungumzia jambo hilo.
Utoaji wa
huduma ya treni jijini hapa imeonekana kuingilia ratiba ya treni za
abiria na mizigo za mamlaka hiyo hivyo kulazimu urekebishaji wa ratiba
za treni hizo.
Mamlaka hiyo inatarajia kubadilisha ratiba ya
treni ya kasi (express) ambayo ilikuwa inaondoka kila siku ya Jumanne
saa 9.50 alasiri na kuwa itaondoka saa 7.50 mchana siku hiyo hiyo na
kwamba hakutakuwa na mabadiliko kwa treni ya kawaida.
No comments:
Post a Comment