WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo watatoa maoni
yao juu ya Katiba Mpya mjini Dodoma, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Tume
ya Mabadiliko ya Katiba kuanza zoezi la ukusanyaji wa maoni ya wananchi,
Mei mwaka huu.
Tangu kuanza kwa zoezi hilo baadhi ya wabunge
wameshatoa maoni yao baada ya Tume hiyo inayokusanya maoni nchi nzima
kufika katika majimbo yao, wabunge hao ni pamoja na Tundu Lissu (Singida
Mashariki) na Shukuru Kawambwa (Bagamoyo).
Zoezi la kukusanya maoni
ya wabunge hao litaongozwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu
Joseph Warioba Makamu wake Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhani, zoezi
hilo litaanza asubuhi.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Iglansoni
wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Jaji Ramadhani ambaye kwa sasa
anaambatana na kundi la tume hiyo lililopo mkoani Singida, alisema leo
itakuwa fursa kwa wabunge kutoa maoni yao.
“Nitakuwa Singida mpaka
ijumaa (jana), kwa sababu Jumamosi (leo) Tume itakuwa mjini Dodoma kwa
ajili ya kupata maoni ya wabunge juu ya Katiba” alisema Ramadhani.
Tume hiyo kwa nyakati tofauti imekuwa ikikutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya kupata maoni yao kuhusu Katiba Mpya.
Makundi hayo ni pamoja na viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama, makundi maalum na sasa ni zamu ya wabunge.
Katika
hatua nyingine Jaji Ramadhani aliwatoa wasiwasi wananchi kwamba sio
lazima waijue Katiba ya sasa, ndio waweze kutoa maoni juu ya Katiba
Mpya.
“Sio kweli kuwa mpaka uijue Katiba ya sasa ndio uweze kuchangia
maoni ya Katiba Mpya, matatizo yanayowakabili wananchi yanahusiana moja
kwa moja na Katiba na ndio hayo mnayotakiwa kuyasema” alisema
Ramadhani.
No comments:
Post a Comment