Saturday, November 3, 2012

MHARIRI wa Gazeti la Business Times, Mnaku Mbani amejeruhiwa kwa risasi

MHARIRI wa Gazeti la Business Times, Mnaku Mbani amejeruhiwa kwa risasi mdomoni na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi akiwa njiani kwenda nyumbani kwake Mbagala, Dar es Salaam.
Mnaku alipigwa risasi juu ya mdomo, upande wa kulia iliyotokea kwenye shavu la kushoto na kupoteza meno matatu ya juu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alisema jana kwamba tukio hilo lilitokea saa 1:20 usiku katika eneo la Mtoni Madafu.
Alisema Mnaku akiwa na watu wengine wanne walikuwa wanasafiri kwenye gari aina ya Toyota Noah wakitokea mjini kuelekea Mbagala, kabla ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kulisimamisha na kuanza kulishambulia kwa risasi wakidhani kuwa lilikuwa limebeba fedha.
“Walikuwa wakipiga risasi wakiwalazimisha watoe fedha, walidhani hili gari lilikuwa likisafirisha fedha kwa hiyo walikuwa na matumaini ya kupata maburungutu ya fedha, walipokosa walianza kutawanyika,” alisema Kamanda Misime.
Alisema miongoni mwa abiria hao wanne, watatu walijeruhiwa kwa risasi na wawili  kati ya hao, walipata matibabu katika Hospitali ya Temeke na kuruhusiwa kurejea makwao, lakini Mnaku alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
“Hatutajua hawa majambazi walikuwa wangapi, lakini tunajua walikuwa zaidi ya watatu, tunachokifanya sasa hivi ni kuwatafuta na kwa namna yoyote ile... Lazima tutawashika,” alisema.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, uongozi wa Kampuni ya Business Times umesema hali ya Mnaku inaendelea vizuri licha ya kutoweza kuzungumza kutokana na maumivu aliyonayo.
“Hali ya Mnaku inaendelea kuimarika na anaendelea kupata uchunguzi wa madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Uongozi wa Makampuni ya Business Times Limited unaendelea kufuatilia hali yake kwa karibu ili kuhakikisha anapata huduma na uangalizi unaostahili,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mhariri Mtendaji wa Majira, Imma Mbuguni.

Wakili apigwa risasi Mwanza
Huko Mwanza, Wakili wa kujitegemea wa Kampuni ya Juristic Law Chamber, Elias Hezron amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando baada ya kushambuliwa kwa risasi tumboni na kuporwa kompyuta ndogo (laptop).
Tukio hilo limetokea siku chache tangu kuuawa kwa risasi kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow kwa risasi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lili Matola amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema jeshi lake linafuatilia tukio hilo na baada ya kukamilisha uchunguzi wake, litatoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, wakili mwingine wa kampuni hiyo, George Hezron ambaye ni kaka yake wa wakili huyo, alisema tukio hilo lilitokea saa nane usiku wa kuamkia jana nyumbani kwa wakili huyo huko Nyegezi, Wilaya ya Nyamagana.
Alisema kabla ya uvamizi huo, umeme ulikatika na kisha wavamizi hao wanaosadikiwa kuwa walikuwa wawili walifanikiwa kuvunja milango ya nyumba anayoishi na kumvamia. Kabla ya kumpiga risasi, walimtaka atoe laptop yake ya ofisi ambayo amekuwa akiitumia kutunzia nyaraka za uwakili pamoja na simu zake za mkononi.
“Wakili aligoma kutekeleza maagizo yao na mmoja wa wavamizi hao alimpiga kwa nondo kichwani, ndipo alipoanza kupambana.  Wakati amefanikiwa kumdhibiti mmoja, mwingine alimpiga risasi ya tumboni na wote kutoweka na laptop hiyo pamoja na simu zake mbili na nyingine za mkewe,” alisema Wakili George.
Alisema kwa sasa hali ya wakili huyo inaimarika licha ya kuwa ICU akiwakariri madaktari waliomweleza kuwa risasi hiyo haikuathiri tumbo lake kwa kiasi kikubwa na kwamba upo uwezekano wa kupona mapema.
Kumekuwa na mfululizo wa matukio ya mauaji ya watu katika Jiji la Mwanza tangu mwezi uliopita. Kabla ya tukio hilo la usiku wa kuamkia jana, Oktoba 13, mwaka huu saa nane usiku, watu wasiojulikana walimuua Kamanda Barlow katika mazingira ambayo bado hayajafahamika chanzo chake. Tayari watu watano wameshafikishwa mahakamani wakikabiliwa na kosa hilo.
Oktoba 9, mwaka huu Ofisa Uhamiaji katika Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Mwanza, Albert Buchafwe alinusurika kuuawa kwa risasi baada ya kushambuliwa na polisi saa nne usiku eneo la Nyakato, katika kile kilichodaiwa kuwa jeshi hilo lilikuwa likishambulia majambazi.

No comments:

Post a Comment