Saturday, November 3, 2012

Wazee Kyela watoboa ukweli kuhusu Ziwa Nyasa

WAKATI nchi ya Malawi ikiendelea kushikilia msimamo wake, kuwa mpaka Mashariki mwa Ziwa Nyasa kati yake na Tanzania unatenganishwa na ardhi ya Tanzania, Wazee wilayani Kyela, wametoboa siri na kuweka hadharani ukweli wake.
Wazee wengi waliotoa ushahidi juu ya ukweli wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi ndani ya Ziwa nyasa,  mbele Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe  walisema Malawi inasababisha chokochoko isiyo na msiongi.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mstaafu, John Mwakipesile (70), ambaye alikuwa wa kwanza, kuzungumzia suala hilo, alisema anashangazwa na madai hayo mapya  ya Malawi kuwa Ziwa lote  ni  miliki yao.
Alisema kitendo hicho cha nchi hiyo kukurupuka kinapaswa kupuuzwa kwa kuwa  jambo hilo halina ukweli na linapingana na historia na desturi za kweli za maisha ya kawaida ya wananchi wa mpakani wa mataifa haya toka enzi za ukoloni.
Alisema madai ya Malawi hayajazingatia historia ya kweli ya ziwa hilo kwani madai yao  yote ni kujaribu kuficha ukweli kwa kuwa  yeye  kama kizazi cha tatu hata siku moja hakuwahi kusikia kuwa ziwa lote ni mali ya nchi hiyo.
Alisema kuna ushahidi wa kutosha juu ya Tanzania kuwa miongoni mwa wamiliki wa ziwa hilo, kwani kuna mali  za Watanzania yakiwamo makaburi ndani ya ziwa hilo baada ya kumezwa.
Alitolea mfano shule ya msingi  aliyosoma katika  mwaka 1945  kuwa ilishamezwa na ziwa hilo, yakiwemo majengo ya baraza (Mahakama) katika kijiji alichozaliwa cha Mwaya katika wilayani humo.
“Mimi kwa umri wangu wa miaka 70 ni kizazi cha tatu katika wilaya hii nakumbuka shule niliyosoma mwaka 1945 pale Mwaya nilipozaliwa ilishamezwa na Ziwa na ni umbali wa kilomita mbili toka pwani ya sasa kijijini hapo” alifafanua Mwakipesile.
Naye Maini Mwakisambwe (83), Mkazi wa Kata ya Katumba songwe, alisema tangu azaliwe alikuwa akijua mpaka  ni Mto Songwe ambao unaingiza maji ndani ya ziwa hilo  na ndio uliotumika kama mpaka wa kuligawa ziwa kwa mataifa haya mawili.
Mbali na hilo, lakini pia wakiwa vijana walishuhudia viongozi wa Serikali zote mbili wakiheshimu mpaka huo ndani ya ziwa , kwa kuwa hata waliposafiri toka upande mmoja kwenda mwingine kila wakifika eneo la Mto Songwe bendera ya upande mmoja ilishushwa na kupandishwa ya upande mwingine.
Philipo Mwandemele(73) kabla ya kuanza kutoa maelezo yake alitoa  kitabu kimoja kinachozungumzia maisha na desturi za wakazi wa nchi hizi mbili kama nyaraka muhimu  inayoweza kutumika kueleza ukweli juu ya sakata hilo la mpaka.

No comments:

Post a Comment